Jun 22, 2024 06:50 UTC
  • Uanachama katika shirika la BRICS kuwekewa masharti

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametangaza masharti mapya kwa nchi zinazotaka kujiunga na jumuiya ya BRICS.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov amesema kwamba nchi yoyote inayotaka kujiunga na kundi la BRICS haipaswi kushiriki katika "vikwazo haramu vya upande mmoja" dhidi ya nchi zingine.

Russia ilianzisha kundi la BRICS mwaka 2009 na kwa sasa kundi hili lina asilimia 42 ya watu wote duniani, 30% ya jiografia ya dunia na 24% ya pato la uchumi wa dunia.

Kundi hili la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi, ambalo hadi hivi karibuni lilikuwa na wanachama wakuu watano tu, yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, lililipanuka zaidi Januari mwaka huu baada ya Iran, Ethiopia, Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu kujiunga na kundi hilo.

Saudi Arabia pia imealikwa na iko tayari kuwa mwanachama. Mataifa mengine mengi kadhaa yameonyesha nia ya kujiunga huku mengine yakiwa tayari yameshatuma maombi rasmi.

Kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), BRICS kwa sasa inachangia kiasi cha 36% ya Pato la Taifa la Kimataifa katika suala la usawa wa uwezo wa kununua (PPP), ikilinganishwa na takribani 30% ya kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiuchumi.

Tags