Russia: Badala ya Ulaya kuzungumzia hali ya Iran ifuatilie kuiokoa Greenland
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema, badala ya viongozi wa Umoja wa Ulaya, EU kutoa matamshi ya kuzungumzia hali ya Iran, ingekuwa bora kama wanegejikita kushughulikia kadhia ya Greenland, ambayo sasa hivi Marekani inafanya juu chini kuitia mkononi.
Zakharova ameeleza hayo katika mahojiano na Idhaa ya Sputnik na akaongezea kwa kusema: "mimi nina suali la kuwauliza viongozi wa Ulaya; je, wanajua Greenland iko wapi au Iran, takribani iko wapi?"
Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameendelea kuhoji: "je wao watu wa Ulaya hawataki kujiuliza, kwa nini wanatoa maoni kuhusu hali ya Iran ambayo iko katika sehemu tofauti kidogo ya dunia, na mbali kidogo na Greenland? Kwa nini Umoja wa Ulaya unashughulishwa na Iran kiasi hiki na unaipa umuhimu mdogo Greenland?"
Zakharova ameuliza tena akimuelekea mtangazai wa Sputnik: "kwa nini wao sasa hivi hawaelekezi juhudi zao zote Greenland? Wewe huhisi kama hali ya Iran imetumiwa kama kisingizio cha kuwaokoa viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa kuwababaisha watu wao na kuwaweka mbali na ukweli kwamba kisiwa chao kinachukuliwa sasa hivi bila kura ya maoni?"
Akizungumzia misimamo ya EU, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema: "EU inaunga mkono waziwazi machafuko nchini Iran."
Huku akibainisha kwamba sheria na kanuni za kimataifa hivi sasa zinatoweka, Zakharova amesema: "vitendo vya Umoja wa Ulaya ni mfano hai wa uungaji mkono wa waziwazi wa machafuko."
Aidha, amesisitiza kwa kusema: "muelekeo wa Umoja wa Ulaya kuhusu maandamano nchini Iran ni wa kinafiki."
Mwanadiplomasia huyo wa Russia amekumbusha kuwa: "katika maandamano ya upinzani nchini Iran, Umoja wa Ulaya unatafuta njia ya kuiwekea mashinikizo nchi hiyo, lakini wakati wa maandamano ya "vizibao vya njano" katika Umoja wa Ulaya, walilaani vitendo vya waandamanaji."
Zakharova ameelezea pia kushangazwa na kauli za hivi karibuni za mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaya Kallas, kuhusu hali ya mambo nchini Iran, na akasema: "uungaji mkono unaodaiwa kuwa wa "kidiplomasia" wa "kuanguka serikali" umekwenda mbali na kuvuka mipaka yote".../