Jun 21, 2024 08:01 UTC
  • Kamanda: Iran itatoa jibu mwafaka kwa tishio la aina yoyote

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu leo hii ina nguvu zaidi kwenye sekta ya ulinzi kuliko wakati wowote ule, na kwamba tishio lolote dhidi ya taifa hili litapata jibu mwafaka na madhubuti.

Brigedia Jenerali Alireza Sabahifard alitoa indhari hiyo jana Alkhamisi, alipokitembelea Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Shiraz kusini mwa Iran, kutathmini utayarifu wa jeshi la anga la Iran katika kujihami na kuzuia vitisho vya maadui.

Ameeleza bayana kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran havitoanzisha vita lakini vitatoa jibu kali na lenye nguvu kwa chokochoko ya aina yoyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Alireza Sabahifard amebainisha kuwa, Tehran itajibu kwa nguvu maradufu uchokozi wowote wa kijeshi dhidi ya ardhi na maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la Iran amesisitiza kuwa, shambulio lolote litakalofanywa dhidi ya ardhi ya Iran, maslahi yake, au raia wake ndani na nje ya mipaka litakabiliwa na jibu kali na madhubuti.

Maafisa wa Iran wameweka wazi kuwa hawatayumba katika juhudi zao za kuimarisha uwezo wao wa kiulinzi, ikiwa ni pamoja na uwezo wao wa makombora na kubainisha kwamba, hatua hizo zimekusudiwa kwa ajili ya ulinzi pekee na kwamba uwezo wa kiulinzi wa nchi hautawahi kujadiliwa.

Tags