Iran yatoa onyo kali kwa Israel dhidi ya vita na harakati ya Hizbullah
-
Amir Saeed Iravani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeionya Israel kuhusu matokeo mabaya ya kuanzisha vita vya pande zote dhidi ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Ujumbe wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa umesema katika taarifa yake siku ya Ijumaa kwamba utawala katili wa Israel utakuwa ni "mpotezaji mkuu" wa hatua zozote za kijeshi dhidi ya Lebanon.

"Vita hivi vitakuwa na mshindwa mmoja wa mwisho, ambaye ni utawala wa Kizayuni wa Israel. Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, ina uwezo wa kujilinda yenyewe na kuilinda Lebanon, labda wakati wa kujiangamiza utawala haramu umewadia," alisema mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa .
Taarifa hiyo imesema Hizbullah ina uwezo wa kujilinda yenyewe na kuihami Lebanon.
Pia imetoa onyo kali kwa hatua zozote za utawala haramu wa Israel dhidi ya Lebanon zinaweza kulitumbukiza eneo la Magharibi mwa Asia katika mzozo mpya.
"Uamuzi wowote wa kipumbavu wa utawala unaoikalia kwa mabavu Palestina wa kutaka kujiokoa unaweza kulitumbukiza eneo la Magharibi mwa Asia katika vita vipya, ambavyo matokeo yake yatakuwa uharibifu wa miundombinu ya Lebanon na vilevile maeneo yanayokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1948", imesema taarifa hiyo.
Jumatano iliyopita, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah, aliapa kwamba "hakuna sehemu" katika maeneo yanayokaliwa na Israel itakayosalimika na makombora yetu ikiwa vita vikubwa vitaanza.
Sayyid Hassan Nasrallah alisisitiza kuwa shambulizi katika eneo la al Jalil (Galilaya) ni chaguo lililoko mezani iwapo utawala haramu wa Israel utavamia kusini mwa Lebanon.
Vilevile alisema kuwa, Hizbullah itashambulia nchi nyingine yoyote katika eneo hili itakayoisaidia Israel dhidi ya Lebanon, akitolea mfano Cyprus, ambayo imekuwa mwenyeji wa majeshi ya utawala katili wa Israel kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi.