Jun 22, 2024 10:54 UTC
  • Masuala ya kiutamaduni na wanawake; ajenda kuu ya mdahalo wa wagombea wa uchaguzi wa rais wa Iran

Mdahalo wa tatu wa kisiasa kwa njia ya televisheni wa wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umefanyika huku wagombea wakibainisha mipango yao ya sera za serikali kuhusu wanawake na uzalishaji wa kiutamaduni nchini.

Katika mdahalo huo wa tatu ulioendeshwa kwa njia ya televisheni, wa wagombea wa duru ya 14 ya uchaguzi wa rais wa Iran ambao ulifanyika jana usiku, wagombea sita yaani Masoud Pezeshkian, Mostafa Pour Mohammadi, Saeed Jalili, Ali Reza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Qazizadeh Hashemi na Muhammad Qalibaf walibainisha na kuweka wazi mipango yao ya utendaji kuhusu wanawake, masuala ya utamaduni na sanaa. Katika mpango wa saba wa miaka mitano wa maendeleo ya Iran kwa lengo la kuimarisha masuala ya utamaduni katika jamii, kunyanyua utambulisho wa kitaifa na ari ya muqawama na vile vile kuimarisha mtindo wa maisha wa Kiislamu na Kiirani; filamu 20 za ubora wa juu zinapaswa kutayarishwa kila mwaka hapa nchini mbali na ongezeko la viwango 25 vya ukuaji wa wastani wa taasisi za kitamaduni na kisanii nchini.

Katika mdahalo wa wagombea wa kiti cha urais wa Iran wa jana usiku, Mustafa Pour Mohammadi Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani amesema kuwa katika sera ya utamaduni atatekeleza mtindo usio wa moja kwa moja na kuunga mkono sera hiyo,  huku Muhammad Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge)  akisema kuwa kipaumbele chake cha awali kitakuwa kuondoa vizuizi na masuala yote yanayokwamisha kazi za wasanii na kwamba serikali itaunga mkono uzalishaji wa kazi za sanaa. Masoud Pezeshkian mgombea mwingine wa kiti cha urais ambaye ni mbunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu pia ameeleza kuwa mpango mkubwa unapasa kuwa katika uzalishaji wa kitamaduni kwa sababu adui anataka kuibua vizuizi na ukwamishaji katika nyanja za kiutamaduni na kisanii za Iran. Katika upande mwingine, Saeed Jalili, Katibu wa zamani wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria historia na ustaarabu wa kale wa Iran na kusema kuwa, serikali chini ya uongozi wake itaomba msaada wa wataalamu wa sekta hiyo ili kusogeza mbele malengo ya kiutamaduni. 

Saed Jalili, mgombea wa kiti cha urais 

Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi Mkuu wa Wakfu wa Mashahidi na Masuala ya Maveterani wa Vita ameeleza wazi mipango yake kuhusu masuala ya kitamaduni na kusema: "Utamaduni wetu unashambuliwa na maadui na tutajaribu kuzindua barabara ya hariri ya kiutamaduni". Wakati huo huo Meya wa mji wa Tehran, Alireza Zakani amesema serikali yake itafuatilia na kushugulikia suala la kuwasaidia wasanii na kuanzisha mfuko wa mikopo ya sanaa. Katika mdahalo huo wa jana usiku, wagombea wote sita wamesisitiza mchango na umuhimu wa  wanawake katika kufanikisha malengo ya jamii na uungaji mkono wa serikali kwa kundi hilo. Midahalo miwili iliyosalia kati ya wagombea sita wa kiti cha urais imepangwa kufanyika Jumatatu na Jumanne wiki hii huku ajenda kuu zitakazojadiliwa zikiwa ni masuala ya kisiasa na kiuchumi kwa utaratibu. Uchaguzi wa kabla ya wakati wa duru ya 14 ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia kufa shahidi mwezi jana Rais Sayyid Ebrahim Raisi na wenzake aliokuwa nao pamoja katika ajali ya helikopta kaskazini magharibi mwa Iran utafanyika Ijumaa tarehe 28 mwezi huu wa Juni.

Shahidi Rais Ebrahim Raisi 

Kwa sababu hiyo, kampeni za wagombea wa kiti cha urais zimeanza nchini tangu tarehe 10 mwezi huu wa Juni baada ya Baraza la Kulinda Katiba kuwaidhinisha wagombea sita. Sehemu ya vipindi vya matangazo ya kampeni za wagombea ni kushiriki kwao katika midahalo  inayorushwa hewani kwa njia ya televisheni inayoandaliwa kwa ushirikiano na vyombo vya habari vya taifa. Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kitengo cha Utafiti cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaonyesha kuwa karibu nusu ya watazamaji wameweza kuwaelewa na kuwafahamu vizuri wagombea baada ya midahalo. Uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuwa baada ya midahahalo kadhaa kufanyika, idadi ya wale ambao walikuwa na shaka na kusita kuhusu ni mgombea yupi wanapasa kumchagua imepungua kwa takriban asilimia 2. Tukiangalia majina ya wagombea sita waliopasishwa kuwania kiti cha rais tunaona kuwa shakhsia hao wanatoka katika mirengo na makundi mbalimbali ya kisiasa. Mbali na  hili, kila mgombea ana uzoefu wa miaka kadhaa ya utendaji katika nyadhifa muhimu za uongozi na serikalini. Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kupasishwa wagombea na kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi  alieleza kuwa, suala la maadili linapaswa kuwa mstari wa mbele kwa wagombea katika kampeni za uchaguzi. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi wagombea kuzingatia maadili kabla na katika uchaguzi na kuwaonya kutougeuza uchaguzi huo kuwa uwanja wa kutunishiana misuli ya kuwania madaraka na kuvunjiana heshima kama ilivyozoeleka huko Marekani na katika baadhi ya nchi za Ulaya. Inatazamiwa kuwa, wananchi wa Iran Ijumaa ijayo Juni 28 watashiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika vituo vya kupig a kura katika duru ya 14 ya uchaguzi wa rais ili kudhihirisha shukrani zao kwa kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya 13 na pia kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali mpya watakayoichagua.  

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu 

 

Tags