Mbunge akamatwa kwa "uchochezi" kuhusu ajali ya ndege nchini Malawi
Polisi nchini Malawi wamemkamata Mbunge, Kamlepo Kalua, na mwanaharakati, Bon Kalindo, kutokana na maneno waliyoandika kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na ajali ya ndege iliyotokea Juni 10 iliyoua Makamu wa Rais wa nchi hiyo Saulos Chilima na maafisa wengine wanane.
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Malawi, Peter Kalaya amethibitisha kukamatwa watu hao akisema kwamba walikuwa wametuma vitu vya "uchochezi kwenye mitandao ya kijamii ambavyo vimejaa uongo na uzushi."
Katika sehemu moja ya taarifa yake, Kalaya amesema, vidokezo vya sauti vilivyosambazwa na watu hao vina mambo makubwa ya uhalifu kwa mujibu wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki na Usalama wa Mtandao.
Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi la Malawi aidha amesema kuwa matamshi ya watu hao yanaweza kuchochea ghasia na fujo.
Kalua na Kalindo wametumia mitandao ya kijamii kuhoji na kupinga maelezo ya serikali kuhusu chanzo cha ajali hiyo ya ndege iliyopelekea kupoteza maisha Naibu Rais.
Ndege hiyo ya kijeshi aina ya Dornier 228 mali ya Jeshi la Ulinzi la Malawi, ilianguka Juni 10 katika msitu ulioko kilomita chache kutoka ji wa Mzuzu kaskazini mwa Malawi kutokana na hali mbaya ya hewa kama alivyotangaza Katibu wa Rais na wa Baraza la Mawaziri wa nchi hiyo, Colleen Zamba.
Tangu wakati huo Rais Lazarus Chakwera wa Malawi amekuwa akiwasiliana na wataalamu wa kigeni ili waungane na Jeshi la Ulinzi la Malawi na Huduma ya Polisi ya Malawi katika uchunguzi wa ajali hiyo ili kujua sababu yake halisi.