Niger yaifutia leseni kampuni ya fueli nyuklia ya Ufaransa
(last modified Fri, 21 Jun 2024 07:44:39 GMT )
Jun 21, 2024 07:44 UTC
  • Niger yaifutia leseni kampuni ya fueli nyuklia ya Ufaransa

Niger imebatilisha kibali cha kuliruhusu shirika moja la nishati la Ufaransa kuendelea kuzalisha fueli nyuklia katika moja ya migodi mikubwa zaidi ya urani duniani.

Shirika hilo la Ufaransa la Orano limetangaza kuwa, limefutiwa kibali cha kuendelea kuzalisha fueli nyuklia katika timbo la Imouraren lililoko kaskazini mwa Niger. Kampuni hiyo ya Kifaransa imekuwepo Niger tangu mwaka 1971.

Inaarifiwa kuwa, mgodi huo wa Imouraren SA una akiba ya tani 200,000 za madini ya urani, ambayo yanatumiwa katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia na silaha za nyuklia.

Mashirika mbalimbali ya Ufaransa yamekuwa yakiwekeza katika miradi ya kiuchumi na migodi katika nchi hiyo ya Kiafrika kwa miaka mingi. Akthari ya miradi hiyo imekuwa ikitekelezwa kupitia mikopo ya muda mrefu.

Uhusiano wa Niger na Ufaransa uliharibika zaidi Julai mwaka jana, baada ya jeshi kumpindua rais ambaye wananchi wa Niger walikuwa wanalalamika vikali kwamba ni kibaraka mkubwa wa Ufaransa, Mohammad Bazoum.

Maandamano dhidi ya mkoloni Mfaransa nchini Niger

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Jeshi la Niger lilitangaza kuwafukuza kikamilifu askari wote wa Ufaransa walioko katika ardhi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi. 

Aidha Januari mwaka huu, ubalozi wa Ufaransa ulifungwa rasmi nchini Niger miezi kadhaa baada ya kufanyika marekebisho ya kisiasa, na Baraza la Kijeshi kuchukua uongozi wa nchi, ambapo lilisisitiza kuondoka vikosi vya kijeshi na kukomeshwa satwa ya Ufaransa katika nchi hiyo ya eneo la Sahel.

 

Tags