May 21, 2024 02:48 UTC
  • Viogozi wa dunia waendelea kuomboleza kifo cha Rais wa Iran

Viogozi mbalimbali wa dunia wameendelea kutoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raisi wa Iran aliyeaga dunia katika ajali ya helikopta.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ametoa salamu zake za rambirambi kwa Iran, baada ya tangazo la kifo cha rais Ebrahim Raisi pamoja na maafisa wengine aliokuwa ameambatana nao akiwemo Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni waa Iran.

Viongozi wengine wa dunia pia wameungana na Michel kutoa pole na salamu zao za rambirambi kwa Iran baada ya rais wake kuaga dunia.

Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amesema, amesikitishwa na vifo vya viongozi hao, akisema bado Malaysia itaendelea kuimarisha mahusiano yake na Iran, kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya watu wao na ulimwengu wa Kiislamu.

Marehemu Sayyid Ebrahim Raisi

 

Naye rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema anamkumbuka Rais Ebrahim Raisi kwa heshima kubwa kutokana na juhudi zake za kuleta amani kwa watu wa Iran na kanda nzima.

Wengine waliotuma salamu zao za pole ni pamoja na Jumuiya ya nchi za kiarabu, Japan, Italia, Pakistan, Srilanka, Jordan Qatar na India.

kwa mujibu wa Ibara ya 131 ya Katiba, Mohammad Mokhbir, (ambaye sasa ni makamu wa kwanza wa rais) atakaimu nafasi ya utendaji ya rais na pia atakuwa na jukumu la kusimamia serikali na kushirikiana na spika wa bunge na mkuu wa idara ya mahakama ili katika kipindi cha siku hamsini zijazo uchaguzi wa rais mpya ufanyike.