May 21, 2024 07:18 UTC
  • Russia yaishambulia US kwa kukosoa waranti wa kukamatwa Netanyahu

Russia imekosoa vikali radiamali hasi ya Marekani kwa ombi la Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), la kutaka kutolewa waranti wa kumtia nguvuni Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia amesema hatua ya Marekani ya kupinga kutolewa waranti dhidi ya Netanyahu inaonyesha unafiki na undumakuwili wa Washington.

Zakharova amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Telegram na kuongeza kuwa: Radiamali ya Marekani inashabihiana na tabia ya nge ambaye amejing'ata, au buibui ambaye amenasa kwenye utando wake.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amesisitiza kuwa, hali ya kuogofya inayoshuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) imetokana na kazi ya wahandisi wa kisiasa wa Marekani.

Netanyahu, mtenda jinai za kivita na waungaji mkono wake

Viongozi mbali mbali wa Marekani akiwemo Rais Joe Biden wamekosoa vikali ombi la Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC) la kutaka kutolewa waranti dhidi ya Netanyahu. Hata hivyo nchi nyingi duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Afrika Kusini, Colombia na hata Palestina yenyewe, zimekuwa zikiishinikiza mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imkamate Netanyahu kwa kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Mashinikizo ya kuitaka ICC imkamate Netanyahu yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Marekani wanaendeleza kampeni kubwa ya kuzuia hatua yoyote ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa kibali cha kukamatwa viongozi watenda jinai na mauaji ya kimbari wa Israel, hususan Netanyahu.

Tags