May 22, 2024 12:46 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi amhutubu Haniya: Ahadi ya Allah ya kutokomezwa utawala wa Kizayuni itatimia

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika mazungumzo na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas na ujumbe alioandamana nao kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kutokomezwa utawala wa Kizayuni itatimia.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatano, Ayatullah Khamenei ameashiria aya za Qur'ani tukufu kuhusu kuthibiti kwa ahadi mbili za Mwenyezi Mungu alizompa mama yake Nabii Musa (a.s.) na kueleza kwamba: sasa hivi ahadi ya kwanza ya Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa Palestina imetimia, nayo ni ya ushindi wa watu wa Ghaza, ambao ni kundi dogo, dhidi ya kundi kubwa na lenye nguvu la Marekani, NATO, Uingereza na baadhi ya nchi nyingine; na kutokana na hayo, ahadi ya pili ambayo ni kutokomea utawala wa Kizayuni inaweza kutimia pia; na kwa rehma za Mwenyezi Mungu itawadia siku ya kuja kuundwa Palestina kuanzia kwenye "Bahari" hadi kwenye "Mto".
 
Ayatullah Khamenei, amezungumzia pia Muqawama wa kipekee wa watu wa Ghaza ambao umewashangaza walimwengu na akafafanua kwa kusema: "ni nani angeamini kama itafika siku zitatolewa nara za kuunga mkono Palestina na kupeperushwa bendera ya Palestina katika vyuo vikuu vya Marekani? Na nani angeamini kama itafika siku yatafanyika maandamano Japan kwa manufaa ya Palestina na kutolewa kwa Kifarsi kauli mbiu ya "Mauti kwa Israel"; na akasisitizia kwa kusema: katika siku za usoni pia yamkini yakatokea matukio kuhusu kadhia ya Palestina, ambayo anaweza mtu leo asiamini.
Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mohammad Mokhber, ambaye kwa mujibu wa Katiba ana jukumu la kushughulikia masuala ya kiutendaji ya Iran, ataendeleza sera na mielekeo ya marehemu Rais Raisi kuhusu Palestina kwa moyo na ari ileile.

 
Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei ametoa shukurani pia kwa taifa la Palestina hususan wananchi wa Ghaza kwa kuungana na taifa la Iran katika msiba wa kufa shahidi Seyyed Ebrahim Raisi; na yeye pia kwa upande wake ametoa pongezi na mkono wa pole kwa Haniya kwa kuuawa shahidi watoto wake na kupongeza subira iliyoonyeshwa na mkuu huyo wa ofisi ya kisiasa ya Hamas.
 
Katika mutano huo, Ismail Haniya, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na ujumbe aliofuatana nao wametoa salamu za pole na rambirambi kwa Ayatullah Khamenei na vilevile kwa wananchi na serikali ya Iran.
 
Akitoa shukurani zake kwa uungaji mkono wa kila mara wa wananchi na serikali ya Iran kwa wananchi wa Palestina, Ismail Haniya amemtaja Shahid Raisi kuwa ni mtu mwenye kuipenda na kuisaidia Palestina na Muqawama na akasema: "marehemu Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, naye pia alikuwa siku zote akiitetea Palestina na Muqawama katika matukio na kwenye taasisi zote kimataifa na mimi nilikuwa nikimwambia mara kadha wa kadha kwamba wewe ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Muqawama".
 
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameelezea pia yanayojiri hivi sasa kwenye medani ya mapambano huko Ghaza na kusisitiza kwa kusema: "leo kambi ya Muqawama katika eneo na vikosi vya Muqawama vya Palestina viko katika hali bora kabisa, na adui Mzayuni yuko katika hali mbaya zaidi, na hii inatokana na rehma za Mwenyezi Mungu.../

 

 

Tags