May 21, 2024 07:20 UTC
  • Iran yatangaza tarehe ya uchaguzi wa rais; Sayyid Raisi kuzikwa Alkhamisi

Iran imetangaza Juni 28, 2024 kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais, kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika ajali ya helikopta iliyotokoea Jumapili katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran.

Tangazo hilo lilitolewa jana jioni, baada kufanyika mkutano wa viongozi wa ngazi za juu wa Iran, uliowaleta pamoja Kaimu Rais, Mohammad Mokhber, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), Mohammad Baqer Qalibaf na Mkuu wa Idara ya Mahakama, Gholamhossein Mohseni Ejei.

Viongozi hao waandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametangaza pia kuwa, usajili wa wagombea wa urais utafanyika baina ya Mei 30 na Juni 3. Kwa mujibu wa Ibara ya 131 ya Katiba, Mohammad Mokhbir, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais atakaimu nafasi ya utendaji ya rais na pia atakuwa na jukumu la kusimamia serikali na kushirikiana na Spika wa Bunge na mkuu wa Idara ya Mahakama ili katika kipindi cha siku 50 zijazo uchaguzi wa rais mpya ufanyike.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Utendaji, Mohsen Mansouri ametangaza Jumatano ya kesho kuwa siku ya mapumziko hapa nchini, kwa ajili ya kuiaga miili ya Sayyid Raisi na maafisa wenzake aliokuwa ameandamana nao.

Wairani wakiwaomboleza viongozi wao

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei anatazamiwa kuongoza Swala ya janaza hapa jijini Tehran kwa ajili ya Mashahidi hao.

Msafara wa kuuaga mwili wa Dakta Raisi unatazamiwa kupitia miji kadhaa ukiwemo mji mtakatifu wa Qum, kusini mwa Tehran kabla ya kuzikwa Alkhamisi katika mji alikokuliwa Mashhad, Mkoa wa Khorasan Razavi, kaskazini mashariki mwa Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi na viongozi kadhaa aliofuatana nao akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir-Abdollahian walikufa shahidi Jumapili katika ajali ya helikopta iliyotokea katika eneo la Varzghan mkoani Azerbaijan Mashariki, wakiwa katika kazi ya kuwahudumia na kuwatumikia wananchi.

Tags