May 05, 2024 12:12 UTC
  • Chama Tawala cha Togo chashinda uchaguzi wa bunge

Chama tawala nchini Togo kimepata wingi wa viti bungeni katika uchaguzi uliofanyika Aprili 29.

Chama cha UNIR cha Rais Faure Gnassingbe kimeshinda viti 108 kati ya 113 katika bunge jipya, kulingana na matokeo ya muda yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Akiwa madarakani kwa takriban miaka 20, Gnassingbe alimrithi baba yake Gnassingbe Eyadema, ambaye alitawala kwa takriban miongo minne katika nchi hiyo ndogo iliyoko katika pwani ya Afrika Magharibi, kati ya Benin na Ghana.

Aprili 19 Bunge la Togo  liliidhinisha mageuzi ya Katiba ambayo yanabadili mfumo wa utawala wa nchi hiyo kuelekea kwenye utawala wa Bunge. Mabadiliko hayo yamekosolewa na vyama vya upinzani vinavyosema kuwa yanamruhusu Rais Faure Gnassingbe kuendelea kung'ang'ania madaraka.

Gnassingbe, 57, tayari ameshinda chaguzi nne, ingawa zote zilidaiwa na wapinzani kuwa na dosari. Kwa mujibu wa katiba mpya, rais wa Togo sasa atachaguliwa na bunge, na sio wananchi, kwa muhula wa miaka minne.

Katiba ya sasa ingemruhusu kiongozi huyo wa Togo kugombea muhula mmoja wa mwisho mwaka wa 2025.