May 24, 2024 10:19 UTC
  • Seneta wa Marekani: Vikwazo vyetu dhidi ya Iran, Russia na China havina tija yoyote

Seneta Rand Paul wa chama cha Republican nchini Marekani amesema sera ya Washington ya kuendelea kushadidisha vikwazo dhidi ya Russia, China na Iran haina tija yoyote.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tass, Paul ameyasema hayo alipohutubia Taasisi ya Quincy ya Serikali Zinazowajibika  (Quincy for Responsible Governments) mjini Washington na kubainisha kuwa sera ya Marekani ya kuendelea kushadidisha vikwazo dhidi ya Russia, China na Iran haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa ya kubadilisha mielekeo ya kisiasa ya nchi hizo.

Katika hotuba yake hiyo, Seneta huyo amesema, amekuwa akiuliza mara kwa mara suali lifuatalo kwa maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje: "hivi mnaweza kuniambia kama kuna mwenendo mmoja tu ambao umebadilika kutokana na vikwazo? Niambieni kama kuna kikwazo kimoja mlichoiwekea Russia kikaifanya Russia iseme: 'tunaomba radhi kwa hilo, haikutupasa kamwe kufanya hivyo. Na tutafanya kile hasa mnachotaka tufanye, tuambieni tu nini cha kufanya na tutafanya.' Au niambieni kama kuna mwenendo mmoja tu ambao umebadilishwa na China, au na Russia au na Iran. Kwa kweli ukiitazama Iran ni kinyume chake hasa".

 
Paul ameongeza kuwa vikwazo havina taathira wala ufanisi wowote, na kwamba kinachofanywa na serikali ya Marekani ni kuongeza tu vikwazo zaidi.
Seneta Rand Paul amesisitiza kuwa badala ya kuweka vikwazo zaidi, Washington inapaswa kuwa na maingiliano ya kidiplomasia na nchi hizo.
Seneta huyo wa Marekani amekosoa pia mpango wa Washington wa kutumia mali za Russia zilizozuiliwa kwa ajili ya kuinufaisha Ukraine na akasema, hatua hizo zinaichochea Moscow tu kuchukua hatua za kulipiza kisasi.../