ICC: Uhalifu wa kivita, jinai dhidi ya binadamu vinaendelea Darfur, Sudan
Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amesema kuna "sababu za kuamini kwamba uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu" unaendelea kufanywa katika eneo la magharibi mwa Sudan la Darfur,
Akielezea uchunguzi uliofanywa na ofisi yake kuhusu mzozo huo mbaya ambao umezuka tangu 2023, Nazhat Shameem Khan ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ilikuwa "vigumu kupata maneno yanayofaa kuelezea kina cha mateso yanayojiri huko Darfur."
"Kwa msingi wa uchunguzi wetu huru, msimamo wa ofisi yetu uko wazi. Tuna misingi ya kuridhisha ya kuamini kwamba uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, umekuwa na unaendelea kufanywa huko Darfur," amesisitiza Naibu Mwendesha Mashtaka huyo wa ICC.
Bi Khan ameendelea kueleza kuwa, ofisi yake ilijikita katika kuchunguza uhalifu uliofanyika huko Darfur Magharibi, kwa kuwahoji waathiriwa waliokimbilia nchi jirani ya Chad.
Ameeleza kwa kina hali "isiyovumilika" ya kibinadamu, huku ikilenga hospitali na misafara ya kibinadamu na kuonya kwamba "njaa inaongezeka" kwa sababu misaada haiwezi kuwafikia "wale wanaohitaji."
"Watu wananyimwa maji na chakula. Ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia vinatumiwa kwa silaha," ameeleza Khan na kuongeza kuwa utekaji nyara kwa ajili ya fidia umekuwa "mazoea ya kawaida".../