May 25, 2024 11:06 UTC
  • UN yaitaka Israel isimamishe mashambulio Rafah kama ilivyoagizwa na ICJ

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutaka utawala haramu wa Israel uheshimu na utekeleza amri ya kusitisha operesheni za kijeshi mjini Rafah, kama ilivyoagizwa na mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa.

Jana Ijumaa, majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) waliutaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe mashambulizi yake katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah na kuondoka katika eneo hilo.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN amesema mkuu huyo wa UN ameitaka Israel ifungumane na amri ya jana ya ICJ, kwa kuwa maamuzi ya mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi yana nguvu za kisheria na yanapasa kuheshimiwa.

Dujarric ameongeza kuwa, Guterres atawasilisha notisi ya amri hiyo ya muda ya ICJ kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Suala la kutekelezwa au kutokelezwa amri ya mahakama, kinachofuata kwetu sisi ni kuendelea na juhudi za kuwafikishia wakazi wa Ukanda wa Gaza misaada ya kibinadamu," amesisitiza Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN

Uamuzi wa jana wa ICJ unaongeza mashinikizo kwa Israel, ambapo tayari Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, Karim Khan ameomba waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Kesi hiyo iliwasilishwa ICJ na Afrika Kusini. Nchi hiyo jana Ijumaa ilisema inafuatilia kuona namna Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakavyojibu uamuzi wa Mahakama ya ICJ, wa kuuamuru utawala wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah, mji ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza ambako ulituma vikosi mnamo Mei 6.


Tags