May 25, 2024 08:12 UTC
  • Kaimu Rais wa Iran azungumza na Mohammad Bin Salman wa Saudi Arabia

Kaimu rais wa Iran Mohammad Mokhber amesema eneo la Asia Magharibi linahitaji sana uboreshaji uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia.

Mokhber aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman siku ya Ijumaa alipokuwa akitoa salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Iran kutokana na kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na waliokuwa nao katika ajali ya helikopta katika mkoa wa kaskazini-magharibi wa Azarbaijan Mashariki siku ya Jumapili.

Mokhber ameutaja uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia kuwa muhimu kwa ulimwengu wa Kiislamu na kusema: "Licha ya upinzani wa baadhi ya madola, uhusiano wetu umefikia kiwango kizuri na eneo hili linahitaji sana uhusiano huo."

Mokhber amesisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi na kuondoa vizingiti ili kukidhi mahitaji ya pande zote mbili ili kuboresha zaidi uhusiano wa kisiasa.

Amesisitiza kuwa, kumpoteza Rais Raisi ambaye alikuwa maarufu na mchapakazi ni jambo chungu lakini hakutaleta mabadiliko yoyote katika njia ya kidiplomasia ya Iran.

Msafara wa mazishi ya Shahidi Raisi jijini Mashhad

Amebainisha kuwa Tehran na Riyadh zitaendelea kustawisha uhusiano wa kidugu kama ilivyokuwa hapo awali.

Kaimu rais wa Iran amesisitiza umuhimu wa kufuata sera ya ujirani mwema na kupanua uhusiano kati ya nchi zote za eneo ili kuwepo utulivu na ustawi wa kikanda.

Aidha Mokhber amemshukuru Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia na Mwanammfalme Bin Salman kwa kutuma salamu za rambirmbi kutokana na tukio hilo la kusikitisha sambamba na kushiriki kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo katika khitma ya kumuenzi marehemu rais na wenzake.

Mohammad bin Salman kwa upande wake amesema Iran na Saudi Arabia zina nafasi muhimu katika eneo na ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa kuboreshwa uhusiano wa pande zote kutaleta mustakbali mzuri. Aidha amebainisha utayari wa Riyadh wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Tehran.

Amesisitiza haja ya kuendeleza njia ya shahidi Rais Raisi ya kuendeleza uhusiano wa pande zote na wa kikanda.

Bin Salman ameongeza kuwa kufa shahidi Rais Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Amir-Abdollahian kumekuwa kuchungu sana kwa Saudi Arabia.