Kikosi cha MONUSCO chaondoka rasmi Kivu Kusini
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO hatimaye kimefungasha virago vyake na kuondoka Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hafla ya kuondoka walinda amani hao wa Umoja wa Mataifa imefanyika katika Kijiji cha Kavumu umbali wa kilomita 33 kaskazini mwa mji wa Bukavu ambapo ameshiriki pia Waziri Mkuu wa Congo DR Judith Suminwa Tuluka.
Mkuu wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasioa ya Congo Bintou Keita ameishukuru serikali ya Kongo kwa ushirika wake katika kufanikisha amani lakini pia amesisitiza kwa mara nyingine kwamba, baada ua Monusco kuondoka, Serikali ya Congo inabaki na wajibu mkubwa kulinda raia wake.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia Mambo ya Ndani Jacquemin Shabani alikiri kuwa hali ya usalama bado ni tete na kuahidi kuwa juhudi zitafanyika kuhakikisha usalama katika jimbo zima la Kivu Kusini. Jacquemin Shabani anaeleza.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kuondoa kikosi cha MONUSCO katika jimbo la Kivu Kusini Jumanne Aprili 30 kwa ombi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba MONUSCO ilianza kusitisha shughuli zake huko Kivu Kusini Januari mwaka huu.
Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.