Jun 24, 2024 11:03 UTC
  • Makubaliano ya kuanzisha mazungumzo kati ya Tehran na Manama, ishara ya mafanikio ya siasa za nje za Iran

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Bahrain zimetoa taarifa ya pamoja zikielezea kuwekwa mikakati muhimu ya kuanzisha mazungumzo baina ya nchi mbili kwa lengo la kuchunguza namna ya kurejesha uhusiano wa kisiasa. Taarifa hii ya pamoja imetolewa kufuatia mazungumzo yaliyofanyika karibuni kati ya Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri mwenzake wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba, ikiwa ni katika fremu ya uhusiano wa kihistoria na kidugu kati ya Ufalme wa Bahrain na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mafungamano yao ya kidini, ujirani mwema, historia na maslahi ya pamoja baina yao, Abdul Latif bin Rashid Al-Ziani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain na Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walikuwa na kikao cha pande mbili siku ya Jumapili, June 23 mjini Tehran kufuatia safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain hapa nchini kwa ajili ya kushitiki katika kikao cha Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia.

Matokeo ya mashauriano ya huko nyuma na utayarifu wa Manama wa kuimarisha uhusiano wake na Tehran, ulipelekea kuanza mazungumzo kati ya viongozi wa Iran na Bahrain ambapo pande hizi zimekuwa zikisisitiza haja ya kuboresha uhusiano wao.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain aliwasili Tehran kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) ambapo pia amekutana na kuzungumza na Ali Bagheri Kani kuhusu uhusiano wa nchi mbili.

Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) ilianzishwa mwaka 2002 na sekretarieti yake iko Kuwait, ambapo nchi 35 za Asia zikiwemo Iran, Thailand, Kuwait, Bahrain, Saudi Arabia, Qatar,  UAE, Oman, Palestine, Kazakhstan, Uzbekistan, Kyrgyzstan na Tajikistan ni wanachama wa Jumuiya hiyo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mwenyekiti wa mzunguko wa jumuiya hiyo tangu mwezi Septemba, mwaka uliopita.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Bahrain 

Katika safari yake ya hivi karibuni mjini Moscow, Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa wa Bahrain alisema kuwa hakuna sababu yoyote ya kuahirisha juhudi za kuhuisha uhusiano na Iran. Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran pia amekaribisha msimamo huo wa mfalme wa Bahrain na kusisitiza kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi za Kiislamu.

Kufuatia kujitokeza baadhi ya tofauti, Bahrain ilimwita balozi wake kutoka Tehran mwaka 2016, na uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukawa umekatika. Hata hivyo kutokana na kuendelezwa siasa chanya za Iran katika eneo, uhusiano wa Iran na Saudi Arabia uliimarika na nchi hizo mbili zikarejesha uhusiano wao wa kawaida wa kidiplomasia, jambo ambalo liliichochea serikali ya Manama nayo kutuma ishara chanya kwa Tehran kwa ajili ya kuanzisha uhusiano. Suala hilo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na maafisa wa nchi mbili.

Mchakato wa mazungumzo ya pande mbili na upanuzi wa ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za eneo uliimarika zaidi katika serikali ya awamu ya 13  ambapo diplomasia athirifu ya Tehran imekuwa na mafanikio makubwa katika kuvutia maoni ya majirani zake. Serikali ya awamu ya 13 ya Iran imechukua mtazamo mpya katika  utekelezaji wa siasa zake za kigeni tangu ilipoingia madarakani tarehe 3 Agosti 2021.

Utekelezaji wa siasa za nje kwa kuzingatia msingi wa kutoegemea nchi za Mashariki wala Magharibi ni moja ya nguzo muhimu katika sera za mambo ya nje ya serikali, ambapo moja ya madhumuni yake muhimu ni kulinda kujitawala kwa nchi katika kudumisha uhusiano na nchi za Mashariki na Magharibi.

Uungaji mkono usio na dosari wa Iran kwa muqawama katika eneo, kutilia maanani ushirikiano na nchi jirani, kuzuia uingiliaji wa kigeni katika masuala ya eneo, kutatuliwa changamoto za eneo na nchi za eneo na kutoa kipaumbele kwa uwezo wa kiuchumi wa ndani ya nchi na kunufaika na uwezo mbalimbali wa majirani ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakitiliwa mkazo na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Msimamo huo wa Iran kuhusu siasa zake za nje hususan katika miaka ya hivi karibuni umevutia hisia za nchi jirani na hivyo kuandaa uwanja wa kuboreshwa na kupanuliwa uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa kieneo.

Kwa maelezo hayo duru mpya ya mazungumzo ya pande mbili kati ya Iran na Bahrain ni ishara ya taathira ya diplomasia ya Tehran katika matukio ya kieneo na kimataifa.