Jun 28, 2024 03:18 UTC
  • Siasa za kindumakuwili za Biden kuhusu vita vya Gaza

Harrison Mann, afisa wa ujasusi katika jeshi la Marekani, ambaye alijiuzulu karibuni katika kupinga uungaji mkono wa Washington kwa utawala wa Kizayuni katika vita vyake vya mauaji ya umati dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza, aliiambia Al Jazeera ya Qatar siku ya Jumanne usiku kwamba: "Kama usingekuwa uungaji mkono wa Marekani kwa Israel, vita vya Gaza visingeliendelea kwa nguvu hizi."

Ingawa utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani unajaribu kuonyesha kuwa unaushinikiza utawala wa Israel ili uruhusu kuingizwa misaada ya chakula katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa, lakini wakati huo huo umeendelea kutoa misaada ya kijeshi kwa Israel bila kusita. Marekani ni muitifaki na muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni katika nyuga za kisiasa, kifedha na silaha. Msimamo huo wa serikali ya Biden umepelekea wataalamu na wajuzi wa mambo kimataifa kusema kuwa siasa za hivi sasa za Ikulu ya White House kuhusu vita vya Gaza ni hatua na doa jeusi sugu katika rekodi yake ya sera za kigeni.

Uungaji mkono wa serikali ya Biden kwa Israeli katika kilele cha vita vya Gaza umekuwa mkubwa kiasi kwamba hata imekuwa ikikwepa ucheleweshaji wa Congress kwa ajili ya kufikisha haraka misaada yake ya kijeshi na kifedha kwa utawala wa Tel Aviv.

Huku Wademokrat wakiendelea kuonyesha michezo yao ya kuigiza na kipropaganda kuwa wanaheshimu haki za binadamu katika vita vya Gaza, hatimaye utawala wa Biden mwezi Mei uliidhinisha utumaji wa mabomu 1,800 ya kilo 900 na mabomu 500 ya kilo 225 aina ya "Mark 84" huko Israel. Kabla ya hapo, wajumbe wenye misimamo huru kidogo wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, kama vile Bernie Sanders, walitoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kupitia upya sheria ya kuipa Israel silaha na kuilazimisha Tel Aviv izingatie viwango vya haki za binadamu kwenye uwanja wa vita. Katika ripoti yake, Wizara ya Fedha ya Marekani ilifichua kuwa katika miezi mitatu ya mwisho ya mwaka uliopita, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilihusika pakubwa katika kupeleka Israel kinyume cha sheria, shekeli bilioni 18 kwa lengo la kuisaidia katika vita dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Takriban shekeli bilioni 7.8 kati ya hizo yaani asilimia 43 yake, zilipewa watengenezaji wa silaha wa Marekani jambo linalothibitisha wazi ni kwa kiwango gani Israel inategemea silaha za Marekani.

Maandamano ya kimataifa ya kulaani jinai za Israel huko Gaza

Aidha suala hilo linathibitisha wazi uingiliaji mkubwa wa Marekani katika operesheni za kijeshi za Tel Aviv katika eneo. Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani, utawala wa Kizayuni umepokea takriban dola bilioni 300 za misaada ya kiuchumi na kijeshi ya Marekani tangu kuasisiwa kwake, na ndiye mpokeaji mkuu wa misaada ya kigeni ya Marekani. Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, msaada wa Marekani kwa Israel unaunda asilimia takriban 15 ya bajeti ya kijeshi ya Israel. Wakati huo huo, tarehe 14 Oktoba, manowari ya pili ya Marekani ikiwa imebeba ndege za kivita aina ya F-16, F-15 na E-10  ilifika katika eneo kwa lengo la kuunga mkono utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina. Katika upande wa pili imekuwa ikishirikiana na waitifaki wake wa Ulaya na wa Kiarabu katika eneo la  Asia Magharibi kwa lengo la kukabiliana na muqawama katika Bahari ya Hindi, unaowasaidia watu wa Ukanda wa Gaza.

Misaada ya Marekani kwa Israel inatumwa katika hali ambayo Sheria ya Leahy ya nchi hiyo, inapiga marufuku kutumwa msaada wa kijeshi kwa serikali za kigeni au makundi yanayokiuka wazi haki za binadamu. Hata hivyo, ili kukwepa sheria hii, utawala wa Biden umedai kwamba umepokea hakikisho kutoka kwa watawala wa Tel Aviv kuwa watalinda maisha ya raia katika vita vya Gaza. Madai hayo yanatolewa katika hali ambayo kwa mujibu wa ripoti zilizopo, tangu Oktoba 7, 2023, jeshi la Israel limedondosha zaidi ya tani 79,000 za mabomu kwenye vichwa vya wakazi wa Gaza.

Kiasi hiki kikubwa cha mabomu ni karibu mara tano zaidi ya mabomu ya nyuklia yaliyodondoshwa huko Hiroshima, Japan mnamo Agosti 6, 1945 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Jinai hiyo imesababisha maafa makubwa ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia, ambapo matokeo yake ni  kufanywa asilimia 85 ya watu milioni 1.9 wa Ukanda wa Gaza kulazimika kuhama makazi yao na kuishi kama wakimbi katika sehemu nyingine za kusikitisha na zisizofaa binadamu kuishi. Katika kipindi hiki karibu Wapalestina 40,000, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa kwa umati na wengine zaidi ya 80,000 wamejeruhiwa. Katika hali hiyo, hapana shaka kuwa Marekani na serikali ya Biden zinashiriki moja kwa moja katika jinai za utawala wa mrengo wa kulia wa Netanyahu kwa kuupa silaha bila masharti yoyote ili uendelee kuwaua kwa umati Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.