Jun 26, 2024 11:50 UTC
  • Canada yazuia Wairani kushiriki uchaguzi wa rais wa Iran nchini humo

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema Wairani walioko katika nchi za Canada na Saudi Arabia hawatapata fursa ya kushiriki uchaguzi wa rais wa mapema unaotazamiwa kufanyika Ijumaa ijayo.

Ahmad Vahidi amesema hayo leo Jumatano hapa Tehran katika mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa, Canada inayodai kuwa kitovu cha haki na mtetezi wa haki za binadamu, imezuia kufanyika uchaguzi wa rais wa Iran kwa Wairani wanaoishi nchini humo.

Kitendo hicho cha Canada cha kuzuia raia wa Iran walioko nchini humo kushiriki zoezi la kidemokrasia ni muendelezo wa hatua za chuki na uhasama za serikali ya Ottawa kwa Wairani.

Hivi karibuni, Canada ilitangaza kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC ) kwenye orodha ya kile inachokiita "makundi ya kigaidi". Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alisema kitendo hicho ni zawadi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, magaidi na maadui wengine wa amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.

Kuhusu kutofanyika zoezi hilo nchini Saudi Arabia, Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema, kwa kuwa Mahujaji 47,000 wa Kiirani hivi sasa wapo katika miji ya Makka na Madina, serikali ya Riyadh haijatoa ushirikiano wa kuwaruhusu raia hao wa Iran kushiriki zoezi hilo, kwa kuwa ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu upo mjini Jeddah.  

Bendera za Saudia na Canada

Hata hivyo amesisitiza kuwa, raia wa Iran wanaoishi nje ya nchi wanaweza kupiga kura zao katika uchaguzi huo wa rais katika vituo 300 vya kupigia kura duniani kote. Aidha amesema Wairani milioni 61 wametimiza masharti ya kushiriki zoezi hilo litakalofanyika katika vituo 90,000 vya kupigia kura.

Uchaguzi huo wa Juni 28 uliitishwa baada ya Rais Ebrahim Raisi kufa shahidi pamoja na watu wengine saba mnamo Mei 19, wakati helikopta iliyokuwa imewabeba ilipoanguka kaskazini magharibi mwa Iran.

Tags