Jun 28, 2024 07:44 UTC
  • Mahakama Kenya yaidhinisha kutumiwa jeshi kukabiliana na waandamanaji

Mahakama nchini Kenya imeidhinisha uamuzi wa kulipeleka jeshi mitaani kuwasaidia polisi, wakati huu maandamano yakiendelea dhidi ya muswada wa fedha wa 2024 ambao serikali imeahidi kuuondoa.

Wakati magari ya kivita ya kijeshi yalionekana Alhamisi mjini Nairobi, mahakama ilitoa uamuzi jana jioni kuwa hatua ya kutumiwa jeshi iliyoidhinishwa na bunge, ni ya halali kutokana na kuzuka kwa machafuko wakati wa maandamano, ambayo polisi wameshindwa kuyadhibiti. Mahakama ilipinga rufaa iliyowasilishwa na chama cha wanasheria.

Jumanne wiki hii, waandamanaji walivamia bunge na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo.

Mashirika ya kiraia yametangaza kuwa, watu 53 wameshauawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano hayo huku jiji la Nairobi likiripoti vifo 30.

 

Waandamanaji Kenya wanamtaka Rais wa nchi hiyo William Ruto ajiuzulu licha ya uamuzi wake wa kuuondoa muswada tata wa fedha wa 2024 uliokuwa umedhamiria kuongeza ushuru ili kusaidia kupunguza mzigo wa madeni nchini humo.

Rais wa Kenya anakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi uliogubika uongozi wake wa miaka miwili; ambapo vijana nchini humo wanaongoza maandamano makubwa ya kupinga ongezeko la ushuru huku wakisisitiza kutekelezwa mageuzi makubwa ya kisiasa.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa kwake na maandamano ya ghasia ya kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 nchini Kenya, yaliyopelekea makumi ya watu kuuawa.

Volker Turk ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi na kuwawajibisha waliohusika na mauaji hayo ya waandamanaji hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, Nairobi.