Muqawama Iraq: Tutashambulia maslahi ya US iwapo Lebanon itavamiwa
(last modified Wed, 26 Jun 2024 02:18:34 GMT )
Jun 26, 2024 02:18 UTC
  • Muqawama Iraq: Tutashambulia maslahi ya US iwapo Lebanon itavamiwa

Katibu Mkuu wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya nchini Iraq ameuonya vikali utawala haramu wa Israel dhidi ya kuingia kwenye vita vipya na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Sheikh Qais Khazali amesisitiza kuwa, maslahi ya kistratajia ya Marekani, muitifaki mkubwa wa utawala wa Kizayuni, yatalengwa na kushambuliwa na makundi ya muqawama katika eneo la Asia Magharibi.

"Iwapo Marekani itaendelea kuunga mkono utawala haramu wa Israel, na adui Mzayuni apanue hujuma zake dhidi ya Lebanon na Hizbullah, basi maslahi ya Washington nchini Iraq na katika eneo (Asia Magharibi) yatakuwa hatarini," amesisitiza Sheikh Khazali.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya nchini Iraq amebainisha kuwa, utawala haramu wa Israel ndiye adui mkubwa zaidi wa ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu, na kwamba harakati hiyo itaendelea kusimama kidete dhidi ya adui Mzayuni.

Katika hatua nyingine, Harakati ya Kiislamu ya Iraq imetangaza kuwa, wanajihadi wa kundi hilo la muqawama wameshambulia maeneo ya kistratajia ya Israel katika mji wa Haifa, ulioko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Wanamuqawama wa wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya nchini Iraq

Tovuti ya habari ya Press TV imeripot habari hiyo na kuongeza kuwa, wanamuqawama hao wa Iraq, usiku wa kuamkia leo, wamefanya operesheni dhidi ya kambi ya kijeshi ya Israeli huko Haifa, kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

Muungano huo wa makundi ya muqawama nchini Iraq  umesema umefanya operesheni hiyo katika muendelezo wa kupinga mashambulizi ya utawala haramu wa Israel, kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza, na kukabiliana na mauaji yanayofanywa dhidi ya raia wa Palestina, wakiwemo watoto, wanawake na wazee.