Sisi katika mkutano na afisa wa US, ataka kusitishwa mapigano Gaza
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi jana Jumapili alitoa wito wa kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita mara moja katika Ukanda wa Gaza, na kuruhusu kuingia misaada ya kibinadamu katika eneo hilo lililozingirwa.
Sisi alitoa mwito huo mjini Cairo alipokutana na Massad Boulos, mshauri mkuu wa Marekani katika masuala ya Afrika ambaye pia mshauri wa rais katika masuala ya nchi za Kiarabu na Mashariki ya Kati, ofisi ya rais wa Misri imesema katika taarifa yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande hizo mbili zilijadili maendeleo ya hivi karibuni katika Mashariki ya Kati na njia za kurejesha utulivu wa kikanda.
Wakati wa mkutano huo, Sisi alizungumzia juhudi za pamoja za upatanishi za Misri, Marekani, na Qatar kwa ajili ya kusitisha mapigano huko Gaza, akithibitisha kujitolea kwa Cairo kuendelea na uratibu wake.
Amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, nchi hiyo ya Kiarabu "inapinga kikamilifu" kufurushwa Wapalestina kwenye makazi yao na kuhamishiwa katika nchi nyingine, na kuvitaja vita vya Gaza kuwa "janga la kibinadamu."
Amesema vita vinavyoendelea Gaza, ambavyo vimeua makumi ya maelfu ya Wapalestina kwa mujibu wa maafisa wa afya katika eneo hilo linaloongozwa na Harakati ya Muqawama ya Hamas, ni tukio ambalo "litatia doa rekodi za historia."
Wapalestina zaidi ya 53,000 wameuawa shahidi katika hujuma za kinyama za Wazayuni tangu Oktoba 2023, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya ya Gaza.