"Makubaliano na US yanaweza kufikiwa Washington ikiacha mashinikizo"
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema mlango wa kufikia makubaliano na Marekani upo wazi iwapo Washington itaachana na tabia yake ya uonevu na sera zake za mashinikizo na kuiburuza Tehran katika mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.
Katika kikao na Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, pambizoni mwa Jukwaa la Mazungumzo la Tehran 2025 jana Jumapili, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitasalimu amri mbele ya mashinikizo.
Dakta Pezeshkian amesisitiza kuwa, Tehran kamwe haitaachana na mpango wake wa amani wa nyuklia, na kwamba haijali mashinikizo au vitisho vinavyoikabili kutoka kwa Marekani.
Katika mkutano huo, Rais wa Iran pia ameeleza matumaini kuwa makubaliano kati ya Tehran na Doha yatatekelezwa haraka, na kuyanufaisha mataifa yote mawili. Aidha amebainisha kuwa, utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya nchi bila shaka utaleta maendeleo chanya katika eneo hili zima la kistratejia.
Bin Jassim Al Thani kwa upande wake, amewasilisha salamu kutoka kwa Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani kwa Rais Pezeshkian, akielezea matumaini kwamba mbinu ya busara ya Rais wa Iran itaimarisha usalama na utulivu katika eneo hili.
Waziri Mkuu wa Qatar amethibitisha uungaji mkono wa muda mrefu wa Qatar kwa haki za Iran, unaotokana na uhusiano wao wa kidini. Vile vile ameashiria kuwa, kwa kuzingatia tajriba za siku za nyuma, mashinikizo na ubabe vimethibiti kutokuwa na tija katika muamala na Iran, huku mazungumzo na maelewano ya pande zote yakiwa na mafanikio.
Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya (Tehran Dialogue Forum) ulianza jana Jumapili na unamalizika leo Jumatatu. Washiriki 200 kutoka nchi 53 duniani wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbalimbali pia wanashiriki katika mkutano huo.