Kuendelea mivutano kati ya Netanyahu na jeshi la Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i113334-kuendelea_mivutano_kati_ya_netanyahu_na_jeshi_la_kizayuni
Vita vya Gaza vimeingia katika mwezi wa tisa huku mizozo na mivutano kati ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na maafisa wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni ikiendelea kushika kasi.
(last modified 2024-06-25T08:51:25+00:00 )
Jun 25, 2024 08:51 UTC
  • Benjamin Netanyahu
    Benjamin Netanyahu

Vita vya Gaza vimeingia katika mwezi wa tisa huku mizozo na mivutano kati ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na maafisa wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni ikiendelea kushika kasi.

Takriban mwezi mmoja uliopita, Yoav Galant, Waziri wa Vita wa utawala unaoikalia kwa mabavu Quds alitangaza upinzani wake dhidi ya amri za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusiana na uendeshaji wa Gaza baada ya vita na kusisitiza kuwa, yeye anapinga utawala wowote wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Katika mahojiano yake na Kanali ya 13 ya utawala ghasibu wa Israel, Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la utawala huo pia amelikosoa baraza la mawaziri la Israel na usimamizi wake usio na tija katika vita vya Gaza na kusema: "Kuzungumzia kuangamizwa Hamas ni hadaa." Hamas ni itikadi iliyopandwa katika nyoyo za watu wa Palestina ambayo haiwezi kukanushwa, na yeyote anayefikiri tunaweza kuitokomeza Hamas anakosea.

Matamashi na kubainishwa mitazamo hii kunaonyesha wazi juu ya kuweko tofauti, migongano na mifarakano ndani ya baraza la mawaziri, haswa kati ya jeshi na maafisa wa wizara ya vita na waziri mkuu na wajumbe wa baraza la mawaziri la Tel Aviv. Tofauti hizi hata zilisababisha Netanyahu kutoa matamshi makali dhidi ya jeshi na kuwakumbusha wakuu wa kijeshi kwamba, Israel serikali yenye jeshi na sio jeshi lenye serikali.

Netanyahu na Yair Lapid

Kadhalika ofisi ya Netanyahu imewahutubu maafisa wa jeshi kwa kuwaambia, jeshi haliwezi kuwa na utendaji na sera tofauti kuhusiana na vita vya Gaza ambazo ni kinyume na maamuzi ya baraza la mawaziri, bali linapaswa kufanya mambo kwa mujibu wa yale yaliyopasishwa na baraza la mawaziri.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ilitoa taarifa na kutangaza kuwa, baraza la mawaziri la kiusalama na kisiasa la Israel limetangaza moja ya malengo yake katika vita vya Gaza kwamba, ni kusambaratisha nguvu za kijeshi na udhibiti wa Hamas huko Gaza, na kwa kawaida jeshi hilo pia linapaswa kuhisi kuwa na jukumu katika suala hili.

Mbali na mizozo hiyo, kila upande kuutuhumu upande mwingine kwamba, ulishindwa kukabiliana na oepresheni ya Kimbunga cha al-Aqswa pia ni sababu nyingine iliyochochea tofauti hizo. Yair Netanyahu, mtoto wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, ambaye alikimbilia Miami huko Marekani baada ya vita vya Gaza, alimshambulia Kamanda wa Jeshi la Anga, Tomer Bar na kusema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii kwa kamanda wa jeshi la Israel: Mlikuwa wapi wakati harakati ya Hamas tarehe 7 Oktoba iliposhambulia miji inayozunguka Gaza?

Gazeti la Kiebrania la Ha'aretz liliandika katika uchambuzi wake kwamba: "Jeshi la Israel sasa lina sababu za wazi za kumlaumu Netanyahu kutokana na kuwa katika miezi iliyopita na tangu kuanza kwa vita, Netanyahu hakuacha kutumia kila fursa aipatayo kwa ajili ya kuwashambulia maafisa na makamanda wa jeshi na kuwalaumu kwa kushindwa Israel Oktoba 7 katika operesheni iliyotekelezwa na Hamas.

Mizozo baina ya baraza la mawaziri na maafisa wa kijeshi wa Israel inapamba moto katika hali ambayo, utawala huo ghasibu umo katika vita vya muda mrefu zaidi vya maisha yake ya miaka 76. Kauli hizi zinaonyesha kuweko mpasuko mkubwa ndani ya baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni. Ni kwa muktadha huo ndio maana ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), shakhsia na maafisa wengi wameonya kuhusu matokeo mabaya ya mzozo kati ya maafisa wa kisiasa na kijeshi wa utawala huo, na akthari yao wanamnyooshea kidole cha lawama Benjamin Netanyahu wakieleza kwamba, yeye ndiye chanzo kikuu cha hali hii.