Jeshi la Kenya kuingia mtaani kukabiliana na waandamanaji
Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vitaingia mitaani ili kuhakikisha vinalinda usalama wa watu na mali zao dhidi ya waandamanaji wanaofanya kile alichokiita uhalifu.
Akihutubia Taifa hapo jana Rais Ruto amesema, miundombinu na vyombo vyote vilivyoanzishwa kwa ajili ya kuulinda Umma na Serikali vitasambazwa kulinda usalama wa nchi na kurejesha nchi kwenye hali ya amani"
Rais wa Kenya amesisitiza kuwa, haikubaliki kuona wahalifu ambao wanajifanya waandamanaji wa amani wanafanya ghasia dhidi ya watu, wabunge walioteuliwa na kuinajisi Katiba na kutegemea waachwe huru, tunapaswa kuutenga na kutofautisha uhalifu na demokrasia na uhuru wa kutoa maoni, nitaendelea kuongoza Serikali ambayo itahakikisha inalinda usalama wa raia wote na mali zao.
Ruto ameapa kwamba matukio ya uvamizi wa Bunge aliyoyaita "kitisho kwa usalama wa taifa", kamwe hayatojirudia kwa gharama yoyote."
Kupitia televisheni, Rais William Ruto wa Kenya ameapa kuchukua msimamo mkali dhidi ya "vurugu na machafuko" yaliyoshuhudiwa hapo jana baada ya maandamano ya kupinga mapendekezo ya serikali yake ya kupandisha kodi na ushuru kugeuka kuwa ya vurugu huku akilaani uvamizi wa Bunge.
Waziri wa Ulinzi wa Kenya Adan Duale ameamuru jeshi la nchi hiyo kupelekwa mitaani na sehemu mbalimbali ya nchi kusaidia polisi kukabiliana na kile alichokiita kuwa dharura ya kiusalama.
Wakati huo huo, tayari watu 10 wanaripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa jana Jumanne wakati polisi walipowafyatulia risasi mamia ya waandamanaji waliovamia majengo ya bunge jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, kupinga sheria ya iliyopitishwa na wabunge ya kuongeza ushuru.