May 25, 2024 11:02 UTC
  • Ripota Maalumu wa UN ataka Israel iwekewe vikwazo

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ametoa mwito wa kuwekewa vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel.

Francesca Albanese ametoa mwito huo leo Jumamosi, kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuuamuru utawala wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Albanese ameeleza bayana kuwa, utawala wa Israel hauwezi kuachana na 'uwendawazimu na uchakaramu huu' iwapo jamii ya kimataifa haitauzuia.

Amesema kuna udharura wa kuiwekea Israel vikwazo vya silaha na kusimamisha uhusiano wa kidiplomasia na Tel Aviv mpaka pale itakaposimamisha hujuma zake dhidi ya Rafah.

Amesisitiza kuwa, Israel inafanya mauaji ya kimbari huko Gaza, sambamba na kuwafukuza Wapalestina wa eneo hilo kwenye makazi yao.

Afisa huyo mwandamizi wa UN amekuwa akikabiliwa na mashambulizi na kupokea vitisho vingi tangu alipoanza kazi yake ya kuandaa ripoti kuhusu jinai zinazofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Ripota huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa walimwengu kukabiliana na ukatili wa Israel na kuilazimisha kutii sheria za kimataifa, na kusisitiza kuwa Israel imetumia vibaya sheria za kimataifa za kibinadamu kuhalalisha ukiukaji wa haki za binadamu unaoufanya huko Gaza.

Tags