May 24, 2024 07:55 UTC
  • Upinzani wa Marekani dhidi ya hatua ya nchi za Ulaya ya kulitambua taifa la Palestina

Siku ya Jumatano, Ikulu ya Marekani ailitoa taarifa ya kuunga mkono kwa pande zote utawala haramu Israel na kusema kuwa Rais Biden anaamini kwamba taifa la Palestina linapaswa kuanzishwa kupitia mazungumzo na si kutambuliwa kwa upande mmoja na baadhi ya nchi.

Ikulu ya White House iliongeza katika taarifa hiyo kwamba inaamini kuwa taifa la Palestina linapaswa kuanzishwa kupitia "mazungumzo ya moja kwa moja" kati ya pande zinazozozana.

Mmoja wa wasemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani, ambaye jina lake halijawekwa wazi, alidai katika taarifa kwamba Rais Joe Biden wa Marekani ni "muungaji mkono mkubwa wa suluhisho la serikali mbili," lakini akaongeza kuwa taifa la Palestina halipaswi kutambuliwa "kupitia kutambuliwa kwa upande mmoja" bali linapaswa "kutambulika" kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.

Tamko la Ikulu ya White House limekuja baada ya nchi tatu za Ulaya, Uhispania, Norway na Ireland, kutangaza Jumatano kwamba zitalitambua taifa la Palestina, na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez akasema anatumai nchi zingine za Magharibi "zitafuata mkondo huo.”

 

Jibu la haraka la Marekani kwa hatua za nchi za Ulaya katika uga wa kulitambua taifa la Palestina linaonyesha kutoridhika kwa Washington na washirika wake wa Ulaya ambao wamechukua msimamo ambao ni kinyume kabisa na msimamo rasmi wa Marekani kuhusu taifa huru la Palestina.

Marekani imekuwa ikidai mara kwa mara kwamba taifa la Palestina linapaswa kuanzishwa kwa njia ya "mazungumzo ya moja kwa moja" kati ya pande zinazozozana.

Kwa maneno mengine, serikali ya Biden inaamini kwamba uundwaji wa taifa huru la Palestina unapaswa kutekelezwa kwa njia ya mazungumzo kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hii ni katika hali ambayo Marekani inapuuza  kwa makusudi ukweli muhimu kwamba, hasa baada ya kuundwa baraza la mawaziri lenye misimamo mikali na la mrengo wa kulia la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Januari 2023, suala la kuasisiwa dola la Palestina limetupiliwa mbali na watawala hao. Vinara wa utawala haramu wa Israel hasa waziri mkuu Netanyahu na  Itamar Ben Guer waziri wa usalama wa ndani wanasisitiza kuhusu suala la kuendelea kuwaua kikatili na kuwaaangamiza Wapalestina.

Aidha, katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa Baraza la Mawaziri la Netanyahu, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na utawala huo kuhusiana na kile kinachoitwa mazungumzo ya pande mbili za Palestina na Israel kwa ajili ya kuunda taifa huru la Palestina, na badala yake, Israel imeshadidisha ukaliti  na mauaji dhidi ya watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. Aidha utawala wa Kizayuni ambao sasa umeingia katika mwezi wa nane wa vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi madhulumu wa Gaza, unaendelea kutilia mkazo kuendelea vita hivyo ambavyo vimepelekea kuuawa shahidi Wapalestina wasiopungua 36,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto sambamba na kujeruhiwa wengine zaidi ya 80,000. Israel impuuza hata ombi la washirika wake wa Magharibi la kujiepusha kushambulia Rafah huko Gaza Kusini.

Mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni Rafah

Sasa, kwa kutilia maanani kuwa zaidi ya nchi 143 za dunia zimelitambua taifa huru la Palestina, nchi kadhaa za Ulaya, zikiwemo Uhispania, Norway na Ireland, kwa kuzingatia hatua ya Tel Aviv ya kukataa kufanya juhudi zozote za kutekeleza mpango wa kile kinachotajwa kuwa ‘serikali mbili’ sasa zimeamua kulitambua taifa huru la Palestina.

Nukta muhimu ni kwamba sambamba na hatua za nchi hizo tatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland Michael Marten ametangaza katika mahojiano kuhusu namna nchi za Ulaya zinalipa uzito suala la kusimamisha vita huko Gaza na kuunga mkono taifa huru la Palestina.

Gazeti la Guardian la Uingereza limesema uungaji mkono wa nchi za Ulaya kwa ajili ya kuundwa taifa huru la Palestina una maana ya kuhitimishwa satwa ya Marekani kama kinara wa nchi za Magharibi kuhusu kadhia ya Palestina na kuzidi kutengwa kimataifa utawala haramu wa Israel.

 

Tags