Afrika Kusini kujiondoa katika kundi la G20 wakati wa urais wa Marekani
-
Enoch Godongwana
Waziri wa fedha wa Afrika Kusini, Enoch Godongwana, amethibitisha kwamba nchi hiyo itaachana na ushirikiano wake na kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi duniani G20 wakati wa urais wa Marekani katika kundi hilo.
Akizungumza katika Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos siku, Godongwana ameutaja uamuzi huo kuwa ni "kurudi nyuma kwa muda".
Rais wa Marekani, Donald Trump alisema mwezi Novemba kwamba Afrika Kusini - ambayo mwaka 2025 ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuongoza jukwaa hilo - haitaalikwa kwenye mkkutano ujao utakaoandaliwa na Marekani.
Tangazo lake lilikuja baada ya miezi kadhaa ya mvutano ulioongezeka kati ya mataifa hayo mawili huku Trump akidai kwa uwongo kwamba kulikuwa na mauaji ya halaiki ya wazungu nchini Afrika Kusini.
"Hii si kwa sababu Wamarekani wanaweza kutufukuza kutoka G20, lakini wanashikilia chombo muhimu cha jukwaa hilo" amesema waziri Godongwana.
Amesema anaamini sauti ya Afrika itasikika katika mkutano wa G20 kupitia Umoja wa Afrika na kwamba hadhani kwamba Uingereza, rais wa G20 mwaka 2027, itaitenga Afrika Kusini.
Uhusiano kati ya Washington na Pretoria umedorora kwa kiwango kikubwa kutokana na tofauti za sera za ndani na za kimataifa hasa hatua ya Pretoria ya kuishtaki Isreal, mshirika wa Marekani, katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kutokana na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.