May 25, 2024 11:03 UTC
  • Borrell: Umoja wa Ulaya uchague ama vita au Israel

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema EU inapasa kuweka bayana msimamo wake kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuutaka utawala wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi mjini Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Josep Borrell amesema hayo katika radiamali yake kwa uamuzi huo uliotolewa na ICJ jana Ijumaa na kuongeza kuwa, "EU inakabiliwa na wakati mgumu, kati ya kuunga mkono utawala wa sheria, au kuikingia kifua Israel.

Akihutubia hafla katika chuo cha European University Institute (EUI) huko Florence nchini Italia, Borrell amesema: Tunapasa kuchagua ama kuunga mkono taasisi za kimataifa na utawala wa sheria, au uungaji mkono wetu kwa Israel, na machaguo yote mawili yatakuwa mazito kwetu, je, msimamo wetu utakuwa upi? 

Kadhalika Mkuu wa Sera za Nje wa EU amelaani na kuitaja kuwa isiyovumilika hatua ya Israel ya kuwaondoa kwa lazima raia wa Kipalestina katika mji wa Rafah. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Wapalestina waliolazimika kuihama Rafah mpaka sasa ni zaidi ya 900,000.

Majaji wa ICJ

Utawala wa Kizayuni unaendesha vita na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana; ambapo hadi sasa umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 35,000 na kujeruhi zaidi ya 80,000.

Hivi karibuni, Borrell ambaye amekuwa akikosoa ukatili na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Isarel dhidi ya watu wa Gaza huko Palestina alidokeza kuwa, yumkini nchi nyingine kadhaa za Ulaya zitalitambua taifa la Palestina, na kwamba kuna haja kwa Ulaya kuwa na msimamo mmoja kuhusu kadhia hiyo.

Tags