Maandamano makubwa yafanyika Uhispania kulaani jinai za utawala wa Kizayuni
Maandamano yamefanyika katika miji tofauti ya Uhispania kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni.
Maelfu ya watu kutoka miji tofauti ya Uhispania walifanya maandamano siku ya Jumanne kuunga mkono wananchi wa Palestina na kupinga siasa za viongozi wa serikali ya Uhispania za kutuma silaha kwa utawala ghasibu wa Israel na kufanya biashara na utawala huo ghasibu. Waandamanaji wametaka kukatwa kikamilifu uhusiano kati ya nchi hii ya Ulaya na utawala huo wa Kizayuni.
Maandamano ya wananchi wa Uhispania dhidi ya jinai za utawala ghasibu wa Israel yaliyofanyika chini ya kauli mbiu ya "Simamisha mauaji ya kimbari huko Palestina, komesha biashara ya silaha na uhusiano na Israel" yaliandaliwa na Mtandao wa Mashirika ya Kiraia ya Mshikamano Dhidi ya Uvamizi wa Palestina RESCOP, na kufanyika katika zaidi ya miji 40 ya Uhispania ikijumuisha Madrid, Barcelona, Seville, Granada na Valencia. Mandamano kama hayo yamepangwa kuendelea katika siku zijazo.
Ana Sanchez, Msemaji wa Mtandao Unaounga Mkono Palestina nchini Uhispania amekosoa ukandamizaji wa maandamano ya waungaji mkono wa Palestina katika baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya na kutangaza kuwa moja ya sifa kuu za utawala wa kibaguzi wa Israel ni kunyamazisha sauti za wakosoaji.
Katika miezi ya hivi karibuni, waungaji mkono wa wananchi wa Palestina kote duniani wamekuwa wakilaani jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umefanya mauaji makubwa ya umati katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina. Baada ya hapo, ulianzisha mashambulizi makali kusini mwa Lebanon na kuua idadi kubwa ya raia wa kawaida.
Kimya cha jumuiya ya kimataifa na taasisi za kutetea haki za binadamu kuhusiana na jinai za utawala ghasibu wa Israel kimepelekea kuendelea kuuawa wanawake na watoto wa Palestina na Lebanon kupitia mashine ya vita ya utawala haramu wa Kizayuni.