Iran yawaita mabalozi wa Umoja wa Ulaya kulalamikia tuhuma dhidi ya IRGC
-
Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Tehran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewaita mabalozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya azimio la hivi karibuni la EU linalolenga Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Mabalozi hao waliitwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia siasa pamoja na wakurugenzi wakuu husika, ambapo Iran ilieleza kwa nguvu malalamiko yake dhidi ya hatua za “kichochezi” za Umoja wa Ulaya.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa EU, katika kitendo kinachoonekana kama cha uhasama, walitangaza Alhamisi kuafiki suala la kuweka IRGC kwenye orodha ya “makundi ya kigaidi” ya umoja huo wa kisiasa na kiuchumi wenye wanachama 27.
Tehran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara mchango wa kipekee wa IRGC katika kuondoa ugaidi katika kanda ya Asia Magharibi.
Wakati wa mazungumzo na mabalozi wa Ulaya, maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran wamekosoa vikali uamuzi wa EU, wakiueleza kama “usio na msingi” wakiashiria kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wazi wa kanuni msingi za Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, hasa kuheshimu uhuru wa kitaifa na kutokingilia masuala ya ndani ya nchi.
Wizara hiyo pia imetaja hatua ya EU dhidi ya IRGC kuwa “makosa ya kimkakati” na “tusi lisiloweza kusameheka” kwa taifa la Iran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imekosoa baadhi ya nchi wanachama wa EU kwa “msimamo usiofaa na wa udanganyifu” kuhusu matukio ya kikanda, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mauaji ya halaiki ya Wapalestina, kuunga mkono shambulio la kijeshi la utawala wa Israel dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka jana, na kuunga mkono ghasia za kigaidi dhidi ya wananchi wa Iran mwezi Januari.
Maafisa wa Iran pia walisisitiza jukumu na utendaji wa IRGC kama mlinzi mkuu wa usalama wa taifa la Iran na kama nguvu inayoongoza katika kupambana na ugaidi wa Daesh.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeonya pia kuwa azimio “lisilo halali” la EU linaweka “kigezo hatari” katika uhusiano wa kimataifa, linaangamiza kanuni za sheria, linadhoofisha amani na usalama wa kimataifa na kuharibu ushirikiano katika juhudi za kupambana na ugaidi.
Mabalozi wa EU, kwa upande wao, wamesema watapeleka malalamiko ya Iran kwa serikali zao haraka iwezekanavyo.