May 05, 2024 03:07 UTC
  • Sisitizo la Iran kuhusu Palestina kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa

Amir Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza Jumatano katika kikao cha Baraza Kuu la umoja huo kilichoandaliwa kwa lengo la kujadili kura ya turufu iliyopigwa na Marekani kupinga ombi la Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Iran katika umoja huo, ameunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika umoja huo na kuongeza kuwa hatua isiyo ya uwajibikaji ya Marekani kutumia vibaya kura hiyo katika kupinga haki halali ya Wapalestina, ni kinyume na dhamira ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Iran na aghalabu ya nchi za dunia, utatuzi wa kadhia ya Palestina unawezekana tu kwa kuheshimiwa kikamilifu haki ya taifa hilo ya kujitawala na kuundwa taifa huru la Palestina, mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu. Baada ya kushadidi mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza katika miezi ya hivi karibuni, shughuli za kidiplomasia za kulitambua taifa huru la Palestina na uanachama wake kamili katika Umoja wa Mataifa zimeongezeka. Aprili tarehe 18, wakati wanachama 12 wa Baraza la Usalama, ikiwa ni pamoja na Russia na China, walipopiga kura ya kuunga mkono azimio la kuikubali Palestina kama mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, Marekani ilipiga kura ya turufu dhidi ya azimio hilo.

Taifa huru la Palestina limetambuliwa na nchi 140 kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, na kuna balozi na uwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika nchi 95 za dunia. Kwa ajili hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, inaamini kwamba, kutambuliwa rasmi jambo hilo ni hatua muhimu katika kukabiliana na dhulma za kihistoria dhidi ya wananchi wa Palestina.

Amir Saeid Iravani

Mbali na uwakilishi wa Iran, uwakilishi wa nchi nyingine nyingi, zikiwemo Russia na Pakistan, umesema katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuwa uwanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa kama nchi huru ni moja ya masharti ya msingi na ya lazima katika juhudi za kutatua kwa amani mgogoro wa Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Serikali za Uhispania na Ireland awali ziliwasilisha mpango kwa Umoja wa Ulaya, zikiomba kuungwa mkono na taasisi hiyo kwa ajili ya kutambuliwa rasmi Palestina kama nchi huru katika Umoja wa Mataifa. Palestina kwa sasa ni mwangalizi wa kudumu katika umoja wa huo. Ingawa nchi zenye hadhi ya waangalizi zinaweza kushiriki katika vikao vingi vya umoja huo, lakini hazina haki ya kupiga kura. Kwa hakika kikwazo kikubwa zaidi kwa Palestina kuwa mwanachama wa kudumu katika Umoja wa Mataifa ni upinzani wa serikali ya Marekani. Nchi ambayo kwa upande mmoja inadai kuunga mkono mchakato wa kubuniwa mataifa mawili huru katika mzozo wa Palestina na Israel, lakini wakati huo huo inapinga uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa.

Suala jingine muhimu ni kwamba uungaji mkono wa nchi nyingi za dunia kwa ajili ya Palestina kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa umeongezeka baada ya vita vya Gaza na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, suala ambalo linaweza kutathminiwa kama moja ya matokeo ya jinai za utawala huo wa Kizayuni katika ukanda huo. Kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa, uanachama kamili wa Palestina unahitajia kupitishwa azimio la Baraza la Usalama kwa uungaji mkono wa nchi 9 wanachama, kwa sharti kwamba mmoja wa wanachama wa kudumu wa baraza hilo, yaani Marekani, Russia, Ufaransa, Uingereza na China, asipinge azimio hilo. Licha ya uungaji mkono wa Wamagharibi kwa Tel Aviv na kuvurugwa juhudi za Palestina kuwa mwanachama rasmi na kamili wa Umoja wa Mataifa, lakini hali ya mambo ni kinyume na matakwa yao na ya utawala wa Kizayuni. Kwa kuzingatia hali hiyo, sisitizo na ufuatiliaji wa jumuiya ya kimataifa, unaweza kupelekea Palestina kupewa uanachama kamili katika taasisi hiyo muhimu zaidi ya kimataifa katika siku za karibuni.

Tags