May 05, 2024 12:01 UTC
  • Iran yapongeza uamuzi wa Uturuki kukata uhusiano wa kibiashara na utawala wa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza uamuzi wa serikali ya Uturuki wa kukata uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na utawala wa Kizayuni wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan kando ya kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) mjini Banjul, mji mkuu wa Gambia.
Akilaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Ghaza, Amir-Abdollahian amekumbusha juu ya ulazima wa kuwa na nafasi kubwa na amilifu zaidi ya nchi za Kiislamu hususan Iran na Uturuki katika kuunga mkono suala la Palestina.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aidha ameelezea utekelezwaji wa operesheni yenye nguvu na adhabu iliyopewa jina la Ahadi ya Kweli dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika fremu ya ulinzi halali wa jeshi la Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wa Uturuki pia ameashiria kustawishwa uhusiano na Iran katika nyanja zote kuwa moja ya vipaumbele vya Ankara na kukaribisha kuimarishwa ushirikiano na Tehran katika vikao vya kieneo na kimataifa.

Katika kikao hicho Hakan Fidan ameelezea mtazamo na misimamo ya Uturuki kuhusu matukio ya kieneo, hususan hali ya Palestina kama suala muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu.
 

Tags