May 04, 2024 06:55 UTC
  • Mwendesha Mashtaka ICC akemea vitisho vya Marekani na Israel

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa wito wa kusitishwa vitisho kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo, ikisema kuwa vitisho hivyo vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya mahakama hiyo inayoshughulikia uhalifu wa kivita.

Mahakama ya ICC imetoa tamko hilo baada ya Israel na Marekani kukosoa uchunguzi inaoufanya kuhusu madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Israel kwenye Ukanda wa Gaza.

Ofisi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X kwamba majaribio yote ya kuzuia kazi ya wafanyakazi, kuwatisha, au kuwashawishi isivyofaa lazima yakome mara moja, ikibainisha kuwa Mkataba wa Roma, ambao unafafanua muundo wa mahakama na maeneo ya mamlaka yake, unazuia mwenendo kama huo.

Japokuwa Israel na Marekani hazijatia saini hati ya mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa, lakini ICC inaweza kuwahukumu watu binafsi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu au mauaji ya kimbari.

Wiki iliyopita, Israel ilieleza wasiwasi wake kwamba huenda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inajiandaa kutoa hati za kukamatwa maafisa wa serikali kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu katika vita vya Ukanda wa Gaza.

Viongozi wa Marekani wameanzisha kampeni kubwa ya kuzuia hatua yoyote ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa kibali cha kukamatwa viongozi watenda jinai na mauaji ya kimbari ya Israel, hususan waziri mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu, kwa tuhuma za uhalifu wa kivuita na jinai dhidi ya binadamu.