May 05, 2024 12:04 UTC
  • Kampeni zamalizika kabla ya uchaguzi wa urais nchini Chad

Kampeni zilimalizika nchini Chad Jumamosi kabla ya uchaguzi wa rais wa Jumatatu ili kuhitimisha kipindi cha mpito cha miaka mitatu.

Zaidi ya Wachadi milioni 8 wametimiza masharti ya kupiga kura, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Kusimamia Uchaguzi (ANGE).

Oloy Hassan, afisa mkuu wa ANGE, alitangaza mwishoni mwa juma kwamba hatua zote muhimu zimechukuliwa ili kuhakikisha uchaguzi wa urais unakwenda vizuri.

Matokeo yanatarajiwa kutolewa tarehe 21 Mei.

Wagombea kumi wanashiriki katika uchaguzi huo wa urais, akiwemo Waziri wa Elimu ya Juu Lydie Beassemda, mgombea pekee wa kike.

Lakini, kinyang'anyiro kikubwa kinatarajiwa kuwa kati ya Jenerali Mahamat Idriss Deby, rais wa mpito na Waziri Mkuu Succes Masra.

Deby alichukua mamlaka mnamo 2021 baada ya kifo cha baba yake, Idriss Deby Itno, ambaye alikufa kwenye mstari wa mbele wa vita dhidi ya waasi baada ya kutawala kwa miaka 30.

Anawania kwa tikiti ya chama tawala cha Patriotic Salvation Movement (MPS), kilichoasisiwa na babake, na anaungwa mkono na muungano wa vyama vingine zaidi ya 200.