Apr 27, 2024 02:47 UTC
  • Hamas: Miili ya makaburi ya umati Gaza ifanyiwe uchunguzi

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa wito wa kutumwa timu za uchunguzi ili kutambua miili iliyogunduliwa kwenye makaburi ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.

Harakati ya Hamas imetangaza katika taarifa yake kuwa: Huku timu za madaktari zikiendelea kutafuta miili ya mashahidi waliouawa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na kuzikwa katika makaburi ya umati katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis, tunautaka tena Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine zinazohusika kutuma timu maalumu za madaktari na vifaa vinavyohitajika ili kutafuta maiti za waliotoweka na kutambua miili ya mashahidi katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa hiyo ya Hamas imesema, zaidi ya nusu ya miili 292 ambayo imegunduliwa hadi sasa katika Hospitali ya Nasser, haijatambuliwa.

Maiti zilizofukuliwa katika makaburi ya umati, Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina pia imesisitiza ulazima wa kuundwa mara moja kamati huru ya kimataifa itakayochunguza jinai hiyo ya kinyama.

Mwishoni mwa taarifa hiyo, Hamas imetahadharisha dhidi ya kufumbiwa macho jinai hiyo ya kutisha na kuendelezwa siasa za kuikingia kifua Israel na kuficha jinai zake.

Awali, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu makaburi ya umati yaliyogunduliwa katika hospitali kuu mbili za Ukanda wa Gaza, na kusema kwamba ameshtushwa sana na uharibifu uliofanyika katika wa Hospitali ya Al-Shafa na kituo cha Matibabu cha Nasser.

Israel imeharibu hospitali na vituo vyote vikuu vya matibabu vya Gaza na kuua mamia ya wagonjwa na wahudumu wa afya waliokuwa kwenye vituo hivyo. 

Tags