9 Rabiul Awwal, Siku ya Kuanza Uongozi wa Imam wa Zama
(last modified Thu, 08 Dec 2016 16:43:48 GMT )
Dec 08, 2016 16:43 UTC
  • 9 Rabiul Awwal, Siku ya Kuanza Uongozi wa Imam wa Zama

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kuwa nami katika Makala ya Wiki hii ambayo itazungumzia siku ya kuanza uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwali inasadifiana na siku ya kuanza Uimamu na uongozi wa huja wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi (as). Siku ya kudhihiri Mahdi (as) inayosubiriwa kwa hamu kubwa na walimwengu, itakuwa mwisho wa dhulma na mashaka yote ya mwanadamu. Siku hiyo dhulma na uonevu vitafunga virago na haki na uadilifu vitatawala dunia nzima.    

Imam Mahdi (as) alizaliwa katika siku ya nusu ya mwezi wa Shaaban mwaka 255 Hijria katika mji wa Samurra nchini Iraq. Ni mtoto wa Imam Hassan Askari (as) na Bibi Narjis ambaye baadhi ya riwaya zinasema ni binti Yoshua, mtoto wa Kaisari wa Roma kutoka kizazi cha Sham'un aliyekuwa miongoni mwa Hawaruyyun na masahaba wa karibu sana wa Nabii Issa Masiih (as). Kipindi cha uongozi wa Imam Hassan Askari (as) kilikuwa miongoni mwa vipindi vigumu sana kwa Ahlibaiti wa Mtume (saw). Khalifa Muutamid wa kizazi cha Bani Abbas kwa kutegemea habari zilizokuwa zimemfikia, alijua vyema kwamba, hujja wa mwisho wa Mwenyezi Mungu SW atakayepambana na madhalimu na kuasisi serikali ya uadilifu na Tauhidi kamili kote duniani atazaliwa katika nyumba ya Imam Askari (as). Kwa msingi huo alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, anazuia jambo jambo. Hata hivyo Imam Mahdi (as) alizaliwa kwa uwezo wa Allah na baadaye akaenda ghaiba na kutoweka mbele ya macho ya walimwengu hadi atakaporuhusiwa kudhihiri tena katika kipindi cha aheri zamani na karibu na mwisho wa dunia. 

Kuanza kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama

Imani ya mustakbali mwema na kudhihiri mwokozi wa dunia nzima iko katika dini nyingi na ni itikadi inayozishirikisha karibu dini zote za mbinguni. Dini hizo zinaamini kuwa, mwokozi huyo atadhihiri na kusafisha dunia na dhulma na kueneza uadilifu na haki. Dini za mbingini zinaamini kwamba, utafika wakati ambapo ufisadi, dhulma na uonevu vitaenea na kutawala duniani nzima. Wakati huo ndipo atakapodhihiri mwokozi aliyeahidiwa na kufanya mageuzi makubwa ya dunia na hatimaye kukomesha dhulma, ufisadi na uonevu. Waislamu wanaamini mwokozi huyo aliyeahidiwa kuja kuijaza dunia uadilifu baada ya kujaa dhulma na uonevu, ni mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Mahdi (as). Waislamu wanamwita Mahdi (tunamuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), na Wakristo wanasema mwokozi wa aheri zamani atakuwa Issa Masia (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, wakati Wazartoshi wanasema jina lake ni Sushiant.

Japokuwa Wakristo wanaoshikamana na dini wana imani ya mwokozi aliyeahidiwa, lakini uliberali ambao ndiyo mfumo wa kifikra unaotawala huko Magharibi haukubali itikadi hiyo. Kwa msingi huo maliberali wanasema, itikadi ya kudhihiri mwokozi aliyeahidiwa na ushindi wa haki dhidi ya batili katika kipindi cha aheri zamani ni njozi zisizo na ukweli. Hii ni licha ya kwamba, Mitume wote wa Mwenyezi Mungu walisisitiza fikra hii ya ushindi wa haki dhidi ya batili na kudhihiri mwokozi katika aheri zamani. Itikadi hii pia imesisitizwa na wanafalsafa wengi kwa kutumia hoja za kimantiki.

Wakati huo huo, sifa ya kutoa matumaini mema ya itikadi hii ya kudhihiri kwa mwokozi aliyeahidiwa katika aheri zamani na taathira zake nzuri kwa mtu binafsi na jamii imezidisha wimbi la watu kuamini itikadi hiyo duniani. Hii leo sambamba na kukithiri dhulma, ufisadi, ubaguzi na uonevu katika maeneo mbalimbali ya dunia, fikra na itikadi ya kudhihiri mwokozi aliyeahidiwa pia inaenea na kupanuka zaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, itikadi hii inawapa watu matumaini ya kukomeshwa dhulma na uonevu na kuwahamasisha zaidi kupambana na mafisadi na madhalimu. Kwa msingi huo kwa kuwa mfumo wa ubepari hauwezi kukana mwenendo huu wa kuwepo kasi kubwa ya kuelekea kwenye itikadi ya mwokozi wa aheri zamani, baadhi ya wanadharia wa kimagharibi wamejitahidi kubuni fikra potofu ya "mji timilifu" au Utopia. Kwa kutumia mbinu mbalimbali na nyenzo kama tasnia ya filamu, Wamagharibi wanafanya njama za kupotosha itikadi ya mwokozi wa aheri zamani na kuiarifisha Marekani kuwa ndiyo jamii timilifu na ya uokovu wa mwanadamu.

Kwa hakika jitihada hizi za kutaka kuiarifisha jamii ya Marekani kuwa ndiyo jamii kigezo, timilifu na ruwaza njema ni kichekecho na pengine joki na maskhara. Hii ni kwa sababu, viongozi wa jamii hiyo ni wawakilishi wa mfumo wa ubepari ambo wako tayari kufanya jinai na uhalifu wa aina yoyote duniani kwa ajili ya kulinda na kubakisha hai mfumo huo. Si hayo tu, bali hata katika jamii hiyo hiyo ya Marekani kuna watu wengi wanaoamini kuwa, Issa Masia atarejea katika aheri zamani na kufanya mageuzi na marekebisho katika jamii hiyo na ulimwenguni kote.      

Hapa inatupasa kusema kuwa, katika mazingira ya sasa ya dunia, fikra na itikadi ya kudhihiri mwokozi aliyeahidiwa inakabiliwa na vitisho kutoka pande mbili. Kwa upande mmoja mabepari wenye nguvu na makundi ya madhalimu duniani ambayo yanakutambua kudhihiri kwa mwokozi aliyeahidiwa kwa ajili ya kueneza uadilifu na usawa na kupambana na dhulma na uonevu kuwa ni pigo na tishio kwa maslahi yao haramu, wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, wanazuia kuenea zaidi itikadi hiyo inayozidisha matumaini ya mustakbali mwema wa wanadamu wote au kwa uchache wanafanya jitihada za kupotosha itikadi hiyo. Katika upande wa pili itikadi na fikra ya mwokozi wa aheri zamani kama zilivyo itikadi nyingine takatifu, haikusalimika na upotoshaji na hurafa kama tunavyoona tafsiri zisizo sahihi zinazotolewa kuhusiana na fikra ya kuwepo Imam Mahdi na jinsi ya kumsubiri mwokozi huyo. Kwa mfano tu, huko Marekani kuna baadhi ya watu wanaosubiri kudhihiri tena kwa Nabii Issa Masia wanaosema, kwa kuwa katika kipindi cha aheri zamani na zama za mwisho wa dunia ufisadi na ufuska vitakithiri sana, hivyo kuna ulazima wa kutayarisha uwanja na mazingira ya kudhihiri Yesu Kristo kwa kueneza uifisadi, ufuska na maovu! Tafsiri kama hizo zinaonekana pia kati ya baadhi ya Wakristo na hata miongoni ya baadhi ya Waislamu.

Hivyo basi kuna ulazima wa kurejea katika mafundisho ya Qur'ani na Hadithi sahihi ili kuzuia upotoshaji wa fikra ya mwokozi, kudhihiri na jinsi ya kumsubiri Imam Mahdi (as). Ili kutayarisha mazingira na uwanja mzuri wa kudhihiri Imam wa Zama, Waislamu wanapaswa kujitayarisha wao wenyewe kabla ya jambo lolote jingine. Sharti la kujitayarisha huko ni kujijenga kimaanawi na kiroho na kumjua ipasavyo mtukufu huyo na sifa zake. Kwani mtu anayemjua vyema Imam na kiongozi wake wa zama ataelewa pia kwamba, mtukufu huyo ni mtetezi halisi wa haki na uadilifu na mpinzani wa dhulma, ubaguzi na uonevu. Hivyo mtu anayesubiri kudhihiri mtukufu huyo anapaswa yeye mwenyewe awe mpigania haki na uadilifu na anayepambana na dhulma, ufuska na ubaguzi popote pale anapokuwa.

Msikiti wa Jamkaran, Qum

Mwokozi katika Uislamu ni mkombozi wa walimwengu wote ambaye ataitunuku dunia nzima hali bora na uadilifu kamili wa kijamii. Imam Mahdi (as) ni shakhsia wa dunia nzima ambaye zama zake zinakomesha kabisa mifumo na sura zote za dhulma. Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihii kwake, ni wa mwisho kati ya Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) na kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa kutoka kwa babu yake, yaani Bwana Mtume, atakuja kuijaza dunia haki na uadilifu baada ya kujazwa dhulma na uonevu. Mtukufu huyo atakuja kutimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu SW anayesema katika aya za 105 na 106 za Suratul Anbiyaa kwamba: Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu waliowema. Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.  

Kwa mujibu wa aya hizi za Qur'ani, waja wema wa Mwenyezi Mungu ndio watakaorithi na kushika hatamu za kuongoza dunia nzima. Na kwa mujibu wa tafsiri na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw), suala hilo litatimia wakati atakapodhihiri Imam Mahdi (as) na utawala wa dunia ukashikwa na waja wema wakiongozwa na mtukufu huyo na hatimaye kukomeshwa dhulma na uonevu. Wakati huo mbingu na ardhi vitatoa neema zake zote, utajiri utagawanywa kwa uadilifu na ustawi na maendeleo vitaonekana kote duniani. Kipindi hicho wanadamu watafika katika daraja ya juu kabisa ya kubalehe kiakiri. Uadilifu na usawa vitatawala dunia nzima na hakuna mtu atakayejiona bora au kuwa juu ya mwingine. Vita, uvamizi na mapigano vitatoweka katika uso wa dunia na ulimwengu utakuwa kama msimu mpya wa machipuo.

Hadithi za Mtume Muhammad (saw) zinazozungumzia suala la kudhihiri kwa mtukufu huyo zinaeleza kuwa, wakati huo kila kaumu, koo na kabila litasikia sauti na wito wake kwa lugha yake. Wito wa mtukufu huyo utakuwa wa dunia nzima na utakuwa na taathira ulimwenguni kote. Imam Mahdi (as) atatimiza mchakato wa kuwaunganisha wanadamu wote chini ya kivuli cha Tauhidi na maisha bora ulioanzishwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Katika mantiki ya Uislamu, ubaguzi, dhulma na uonevu ni miongoni mwa sababu kuu za kuporomoka tamaduni mbalimbali, na hapana shaka kuwa, mtu anayeweza kueneza uadilifu duniani ni yule ambaye yeye mwenyewe anaamini, anapigania na kutekeleza uadilifu. Hizi ndizo sifa wanazopaswa kujipamba nazo wafuasi wa mwokozi wa aheri zamani na Imam Mahdi aliyeahidiwa kudhihiri katika zama hizo na kuijaza dunia uadilifu na usawa.

Wanazuoni wakubwa wa Kiislamu kama Tirmidhi na Abu Daud katika sahihi zao na Imam Ahmad katika kitabu cha al Musnad wamenukuu hadithi ya Mtume (saw) inayosema kuwa: Hata kama itakuwa imebakia siku moja tu katika umri wa dunia, basi Mwenyezi Mungu atamleta mtu kutoka katika kizazi changu ambaye ataijaza dunia kwa uadilifu na usawa baada ya kujazwa dhulma na uonevu. Vilevile Muslim katika kitabu cha Sahihi Muslim, Abu Daud, Ibnu Majah na Tabarani ambao ni miongoni mwa maulama wakubwa wa hadithi wa Ahlusunna wamenukuu hadithi ya Mtume (saw) inayosema: Mahdi ni katika kizazi changu kutokana na watoto wa Fatima.