Jumatano, tarehe 14 Januari, 2026
-
Leo katika historia
Leo ni Jumatano tarehe 24 Rajab 1447 Hijria sawa na Januari 14 mwaka 2026.
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita, Ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw).
Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui.
Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake.
Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.

Katika siku kama ya leo miaka 1108 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia.
Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa.
Mwanafalsafa huyo mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.

Miaka 235 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Allamah Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu.
Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala, Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo na kwa wasomi wengine. Akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi, na baada ya hapo akaelekea Najaf.
Msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na alipendwa sana na watu. Sayyid Bahrul-Ulum aliiishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudi Arabiia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa Msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’habu ya Shia.
Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita ulianza mkutano wa Casablanca nchini Morroco. Mkutano huo uliofanyika wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na rais wa zamani wa Marekani Franklin Delano Roosevelt na Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill kama viongozi wa nchi mbili kuu za waitifaki na kujadili mpango wa kushambulia Sicily nchini Italia na nchi za washirika.
Mwishoni mwa mkutano huo wawakilishi wa nchi zilizoshiriki walitoa taarifa ya pamoja ambayo kwa mujibu wake nchi waitifaki ziliapa kuendeleza vita hadi wakati wa kusalimu amri mahasimu wao bila ya masharti.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita maafisa wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walitekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Salah Khalaf maarufu kwa jila la Abu Iyad akiwa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia.
Salah Khalaf alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na kiongozi nambari mbili wa Fat'h baad ya Yaser Arafat.
Mauaji ya viongozi hao wa ngazi za juu wa PLO tena baada ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine yaani Tunisia, yalionyesha kwamba utawala haramu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ile katika suala la kuwaangamiza wapinzani wake.

Siku kama ya leo miaka 15 iliopita, sawa na tarehe 14 Januari 2011 Rais Zainul Abidin Bin Ali wa Tunisia na dikteta wa nchi hiyo alikimbilia Saudi Arabia kufuatia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi.
Kukimbia nchi Zainul Abidin, kulihitimisha utawala wa kiimla uliodumu kwa nusu karne wa Habib Bourquiba pamoja na Zainul Abidin Bin Ali na wananchi wa Tunisia wakaonja ladha ya uhuru. Zainul Abidin aliingia madarakani mwaka 1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi bila umwagaji damu na kumwondoa madarakani Habib Bourguiba aliyekuwa amejitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo. Bin Ali aliiongoza Tunisia kwa mkono wa chuma kwa miaka 23 huku akiendeleza siasa za kutegemea Wamagharibi na kupiga vita Uislamu.
Kujichoma moto kijana mmoja muuza mboga katika kulalamikia dhulma na ukatili wa maafisa usalama wa utawala wa nchi hiyo, kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa Bin Ali na hatimaye kupinduliwa dikteta huyo.
