Mar 24, 2024 02:26 UTC
  • Jumapili, 24 Machi, 2024

Leo ni Jumapili 13 Ramadhani 1445 Hijria mwafaka na 24 Machi 2024.

Siku kama ya leo miaka 1350 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi, liwali katili na dhalimu katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliishi katika kipindi cha Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, na alikuwa mashuhuri kwa kuwatesa na kuwauwa wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi. Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj Thaqafi ni pamoja na kushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba katika mwaka 74 Hijria. ***

Miaka 118iliyopita katika siku kama leo, alifariki dunia mwandishi wa hadithi wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77. Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hadithi ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu ustawi wa sayansi ya mwanadamu. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa mujibu wa baadhi ya hadithi hizo za Jules Verne. ***

Jules Verne

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Msikiti Mkuu wa mji wa Ganja ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Azerbaijan ulikarabatiwa na kufunguliwa upya baada ya kufungwa kwa miaka 70. Msikiti huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1920 na kufunguliwa tena katika muongo wa 80 katika hafla iliyofanyika sambamba na kuswaliwa Swala ya jamaa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, makumi ya misikiti ilikarabatiwa na kutumiwa na Waislamu kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea Urusi ya zamani na katika jamhuri zake na pia kutokana na matakwa ya Waislamu wote wa Jamhuri ya Azerbaijan. ***

Msikiti Mkuu wa mji wa Ganja

Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na maradhi ya kifua kikuu au Tuberculosis. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 daktari Robert Koch daktari na mtafiti wa Kijerumani alieleza uvumbuzi wake wa ugonjwa wa kifua kikuu katika mkutano uliofanyika Berlin Ujerumani na kwa mnasaba huo siku hii ya tarehe 24 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na maradhi ya Kifua Kikuu. ***

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na maradhi ya kifua kikuu au Tuberculosis.

 

Tags