May 06, 2024 02:31 UTC
  • Jumatatu tarehe 6 Mei, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Mei 2024.

miaka 1104 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alizaliwa malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. 

Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. 

Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. 

Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (saw) na kizazi chake kitoharifu hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). 

Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani ya mashairi.   

Abu Is'haq Kesa-i Marvazi

Katika siku kama ya leo miaka 168 iliyopita, alizaliwa Czechoslovakia, Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili na raia wa Austria.

Akiwa na umri wa miaka minne alihamia mjini Vienna akiwa na wazazi wake. Alipofikisha umri wa miaka saba alijiandikisha katika chuo kidogo cha udaktari ambapo akiwa na miaka 29 alitokea kuwa tabibu aliyebobea kutibu magonjwa ya akili.

Baada ya kutibu wagonjwa kadhaa wenye matatizo hayo alipata uzoefu mkubwa suala ambalo lilimsukuma kufanya majaribio kadhaa katika uga huo. Daktari huyo alifanya utafiti na kutwalii matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa ajili hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis. 

Sigmund Freud alifariki dunia tarehe 23 Septemba 1939 akiwa na umri wa miaka 83 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo. 

Sigmund Freud

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya kimaumbile na msomi mkubwa wa Kijerumani, Alexander Humboldt.

Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa. 

Alexander Humboldt

Tarehe 6 Mei miaka 142 iliyopita mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch ilitangaza habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB).

Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimefupisha umri wa zaidi ya watu bilioni moja wiki mbili kabla.

Baadaye Prf Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka. 

Robert Heinrich Koch

Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Prf Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxy inayoshabihiana na Quinine.

Prf Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika.  **

Tags