Afya kwa Wote, Kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Afya
Shirika la Afya Duniani (WHO) ni miongoni mwa taasisi zilizoanzishwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutimiza moja ya malengo yake muhimu yaani kuhakikisha kila mtu anapata huduma za afya na siha.
Tangu mwaka 1950 Umoja wa Mataifa umekuwa ukiadhimisha siku ya tarehe 7 Aprili kama siku ya Kimataifa ya Afya ili kuwakumbusha wanadamu umuhimu wa siha na afya. Tangu wakati huo Umoja wa Mataifa umekuwa ukitangaza nara na kaulimbiu ya kila mwaka ya siku hiyo ya kimataifa na kaulimbiu ya mwaka huu imetangazwa kuwa ni: Huduma ya afya kwa wanadamu wote, kwa kila mtu na kila mahala, Afya kwa Wote (Universal health coverage: everyone, everywhere "Health for All".

Wataalamu wanasema kuwa huduma ya afya kwa watu wote ni hatua muhimu sana ambayo pale inapodhaminiwa huwawezesha watu wa jamii kupata huduma muhimu sana inayohusiana na chanzo na sababu kuu ya vifo. Huduma ya afya ina maana ya kila mtu katika jamii kupata huduma za tiba bila ya mashaka na matatizo ya kifedha. Kwa msingi huo kaulimbiu ya afya kwa watu wote hapa haina maana ya matibabu yanayotolewa mahospitalini pekee bali inajumuisha huduma zote zinazotolewa katika jamii kwa ajili ya kulinda afya na siha za watu wa jamii hiyo kama vile kusafisha mazingira na maeneo yanayotumika kwa ajili ya kuzalisha mbu wanaoeneza magonjwa mbalimbali, suala ambalo huwa na madhara ya kiafya kwa watu wa jamii husika.
Mjadala huu wa huduma za afya kwa umma ni fursa nzuri ya kuwaelekeza walimwengu kwenye umuhimu wa suala hilo katika ustawi endelevu. Hata hivyo ukweli ni kwamba, kutokana na tofauti kubwa iliyopo baina nchi mbalimbali duniani katika suala la utajiri na ustawi wa kiuchumi inakuwa vigumu na wakati mwingine muhali kutimizwa kaulimbiu ya afya na siha kwa umma, kila mahala na kwa kila mtu. Hii ina maana kwamba, dunia itaendelea kuwa na idadi kubwa ya watu wasioweza kupata huduma muhimu za afya. Kwa maneno mengine ni kuwa, hadi sasa zaidi ya nusu ya watu wa dunia hii hawapati huduma za dharura za afya.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, karibu watu milioni mia moja wanasumbuliwa na umaskini mkubwa kutokana na kwamba, wanalazimika kulipia huduma za afya kwa kutumia karibu dola mbili kwa siku. Zaidi ya watu milioni 800 ambao ni sawa na asilimia 12 ya watu wote duniani kwa uchache wanatumia asilimia 10 ya bajeti ya familia zao kwa ajili ya huduma za afya kwa ajili ya nafsi zao wenyewe au watu wa familia zao.
Utafiti uliofanyika umeonesha kuwa, maeneo mengi ya dunia hususan katika nchi zenye rekodi mbaya ya vigezo vya ustawi endelevu yanakabiliwa na changamoto nyingi katika uwanja wa kufikia malengo yaliyoainishwa katika sekta ya afya. Miongoni mwa sababu muhimu zilizotajwa katika uwanja huu ni kutokuwepo usawa katika suala la kuwawezesha watu wote wa jamii kufikia vigezo vya afya. Uchunguzi uliofanyika katika miaka ya hivi karibuni umeonesha kuwa, nchi wanachama katika Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) ambazo zinaunda asilimia 19 ya jamii ya watu wote duniani zinatumia karibu asilimia 85 ya gharama zote za afya ya umma ulimwenguni wakati nchi za Afrika ambazo zinaunda asilimia 10 ya watu wa jamii ya dunia hazifaidiki isipokuwa asilimia 3 tu ya gharama za huduma za afya.
Inafaa kuashiria hapa kwamba, katika tathmini yake ya masuala ya afya duniani, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) hutilia maanani masuala na vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na makadirio ya wastani wa umri wa watu wa jamii, vifo vinavyotokana na maradhi makhsusi na maradhi ya kuambukiza, huduma za afya, mambo hatarishi kwa afya kama shinikizo la juu la damu, utumiaji wa tumbaku na pombe, utumiaji wa maji yasiyo salama, gharama za huduma za afya, ukosefu wa usawa katika kutoa huduma hizo na kadhalika. Shirika hilo la WHO limekuwa likitoa ripoti mara kwa mara kuhusu maendeleo ya nchi 194 wanachama katika sekta ya afya ambazo lengo lake ni kuhakikisha nchi hizo zinafikia kiwango cha juu kabisa cha ustawi endelevu hadi kufikia mwaka 2030.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambulika kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta ya afya ya umma katika miongo ya hivi karibuni. Ripoti mbalimbali za Shirika la Afya Duniani kuhusu hali ya afya nchini Iran kwa kutilia maanani vigezo vilivyoainishwa, zinaonesha kuwa, Iran imepata mafanikio makubwa katika masuala muhimu kama vile kupunguza kiwango cha vifo vya akina mama kwa asilimia 96. Ripoti hizo zinasema Iran inashika nafasi ya kwanza katika eneo la Mashariki ya Kati katika uwanja huo. Shirika la Afya Duniani linasema huduma bora za afya nchini Iran zimepeleka juu matumaini ya kuishi umri mrefu (Life expectancy) na kufikia wastani wa miaka 73.
Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Institute of Health Metrics and Evaluation katika jimbo la Washington huko Marekani inaonesha kuwa, mwaka 2016 Iran ilikuwa na mafanikio makubwa katika vigezo saba kati ya 9 vya Shirika la Afya Duniani ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo kwa umma na afya ya akina mama wakati wa kujifungua. Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa Iran imepiga hatua nzuri katika vigezo kama vya huduma ya maji safi kwa umma na kuzuia magonjwa ya malaria na virusi vya HIV.
Sekta ya afya ni miongoni mwa sekta zinazopewa kipaumbele katika Jamhuri ya Kiislamu na tarehe 21 hadi 27 Aprili hutambuliwa hapa nchini kama Wiki ya Afya na Siha.
Katika kuthamini mchango na juhudi za Iran katika kuboresha sekta ya afya ya umma, Katibu Mkuu wa zamani wa Shirika la Afya Duniani, Margaret Chan aliipongeza Jamhuri ya Kiislamu katika mkutano wa Juni mwaka jana mjini Geneva kutokana na mafanikio yake katika kutimiza malengo ya ustawi endelevu. Bi Margaret Chan alisema katika mkutano huo kwamba: Anaipongeza Iran kutokana na mafanikio yake makubwa katika sekta ya afya na kudhamini rasilimali kwa ajili ya kuboresha afya ya umma na akazitaka nchi nyingine kufuata stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu. Bi Chan pia alitaja mambo kama kupambana na ubaguzi na ukosefu wa usawa katika utoaji wa huduma za afya, kuimarisha ushirki wa taasisi zisizo za serikali, kuzidisha maarifa ya umma kuhusu masuala ya afya na kadhalika kuwa ni miongoni mwa mbinu zilizotumiwa na Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya afya ya umma kwa ajili ya kufikia malengo ya ustawi endelevu.
Kwa kifupi ni kwamba, Iran inafanya jitihada kubwa za kupanua zaidi huduma za afya kwa umma kote nchini kama inavyosisitiza kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya mwaka huu. Suala hili linatajwa na wataalamu kuwa ni hatua muhimu sana katika kufanikisha malengo ya Shirika la Afya Duniani na kuhakikisha watu wote wanapata huduma hiyo wakati na mahala popote wanapoihitajia bila ya kukabiliwa na mashaka au matatizo ya kifedha. Ni matarajio kwamba itafika siku ambapo wanadamu hawatalazimika kuchagua moja kati ya mambo mawili, ama kuwa na afya na siha au kutumia kipato chao kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao mengine ya kimaisha.