Oct 07, 2018 11:51 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, na karibuni kusikiliza sehemu ya sita ya kipindi hiki cha Maswai Kuhusu Tukio la Ashura.

Baadhi ya maswali yanayoweza kuulizwa na wapenzi na wafuasi wa Imam Hussein (as) ni kuwa je, harakati ya Aba Abdillah al-Hussein (as) ambayo ilipelekea kuuawa kwake, familia na wafuasi wake wa karibu ilikuwa na lengo gani? Na je, mjukuu huyo wa Mtume (saw) alipotoka mjini Madina, alikuwa na lengo la kwenda kupambana na utawala wa Yazid, au hakuwa na lengo hilo bali nia yake hasa ilikuwa ni kuondoka mjini hapo kwa madhumuni ya kuepuka vitisho vya vibaraka wa Yazid na kutokubali kumbai mtawala dhalimu na fasidi kama huyo? Tutajaribu kujibu kwa kifupi maswali haya muhimu katika kipidi chetu cha leo, hivyo kuweni pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

Kundi moja la wataalamu wa masuala ya kidini na kihistoria linaamini kwamba lengo la mapambano ya Imam Hussein (as) dhidi ya utawala dhalimu wa Yazid lilikuwa ni kung'oa mizizi ya utawala huo fasidi na kuasisi mahala pake utawala uliosimama juu ya misingi na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na Qur'ani Tukufu. Kuna nukta muhimu hapa nayo ni kwamba iwapo mtu anadhamiria kuanzisha mapambano kwa ajili ya kusimamisha serikali fulani na akakumbana na vizuizi ambavyo vinamzuia kufikia lengo hilo jambo la busara analotakiwa kufanya ni kusitisha mapambano hayo. Imam Hussein (as)  alifahamu vyema kuwa hangeweza kufikia lengo lake tukufu baada ya kusalitiwa na watu wa Kufa na kukabiliana na jeshi la askari 30,000 la Yazid. Hivyo alipokutana ana kwa ana na jeshi la Hurr bin Yazid ar-Riyahi, Imam alianza kulihutubia jeshi hilo kwa madhumuni ya kubainisha lengo la mapambano yake kwa kusema: "Enyi watu! Kila Mwislamu anayekabiliwa na utawala dhalimu ambao unahalalisha haramu ya Mwenyezi Mungu na kuvunja agano lake, kupinga suna na sheria za Mitume, kueneza dhambi, maasi, kuvuka mipaka na kueneza uadui miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mngu, na kuamua kutokabiliana na utawala kama huo ima kwa vitendo au maneno, basi ni haki kwa Mwenyezi Mungu kumpa Mwislamu huyo adhabu (Moto wa Jahannam) kama ile anayompa dhalimu huyo. Enyi watu! Tambueni kwamba hawa (Bani Ummayyia) wameacha kumtii Mwenyezi Mungu na kuamua kumfuata Shetani. Wameamua kueneza ufisadi na kupuuza sheria za Mwenyezi Mungu....."

Karbala

 

Katika zama za Imam Hussein (as) na baada ya kuaga dunia Muawiyya, mtawala aliyeingia kwa nguvu madarakani hakuwa akizingatia hata sheria za msingi kabisa za Kiislamu. Alikuwa akinywa pombe na kueneza hadharani ufuska wa kingono na kimaadili. Alikuwa akisoma mashairi na kutoa matamshi ya dharau, kejeli na ya kupinga mafundisho ya dini ya Uislamu iliyoletwa na Mtume Mtukufu (saw)! Mtu kama huyo ndiye aliyekuwa akijiita kuwa ni mtawala wa umma wa Kiislamu na khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nukta ya pili ni kwamba maazingira yalikuwa yameandaliwa kwa ajili ya kupambana na utawala kama huo fasidi. Kuwa tayari mazingira ya kufanyika mapambano hakukuwa na maana kwamba hakukuwepo na hatari yoyote iliyowakabili walioamua kufanya mapambano dhidi ya utawala huo bali kulikuwa na maana kwamba mazingira ya jamii ya Kiislamu yalikuwa kwa namna ambayo ukweli wa ujumbe wa Imam Hussein (as) ungesikika na kukubalika na watu wa zama hizo na katika kipindi chote cha historia.

Tukitazama kwa makini mapambano ya Imam Hussein (as) tunafikia natija hii kwamba Imam alikuwa na lengo maalumu na tukufu la mbinguni ambalo lingefikiwa tu kupitia mapambano. Lengo hilo la Kiungu lingeweza kufikiwa tu kupitia utekelezaji wa jukumu muhimu la mbinguni, yaani 'kuirejesha jamii ya Kiislamu katika njia sahihi' na 'kukarabatiwa upya mfumo wa jamii ya Kiislamu.' Harakati ya kufikia lengo hilo ilikuwa na moja ya matokeo haya mawili ima 'kusimamisha serikali ya Kiislamu' au 'kuuawa shahidi' katika njia hiyo. Imam Hussein (as) alikuwa amejitayarisha vyema kwa ajili ya matokeo yote mawili. Alikuwa ameandaa utangulizi wa kusimamisha utawala bora wa Kiislamu na vilevile kwa ajili ya kupata daraja ya juu ya kuuliwa shahidi. Tufaradhishe kuwa Imam Hussein (as) hangesimamisha mapambano; katika hali hiyo hangekuwa ila na machaguo mawili; Ima angelazimika kumbai Yazid na kusalimu amri mbele yake au angeamua kutombai na kukimbilia bondeni au juu ya mlima fulani na kukaa kimya huko. Hili lilikuwa pendekezo la watu kama vile Muhammad bin Hanifa na Ibn Abbas. Njia ya kwanza ilifuatwa na watu kama Abdallah bin Umar ambaye hata kama mwanzoni alikataa kumbai Yazid lakini baadaye aliamua kumbai na hakupata lolote ghairi ya kudhalilishwa. Njia ya pili ilifuatwa na Abdallah bin Zubair ambaye aliamua kukimbia na kujificha kwenye al-Kaaba. Badala ya yeye kuilinda nyumba hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu, aliifanya nyumba hiyo kuwa ngao ya kumkinga yeye, ambapo nyumba hiyo ililengwa na kuharibiwa kwa mizinga ya maadui wa Mwenyezi Mungu. Yeye pia hakuwa na mwisho mwema ila wa kudhalilishwa.

Kutokana na matukio hayo mawili ya kihistoria, tunajifunza kwamba njia iliyochaguliwa na Imam Hussein (as) ya kukabiliana na dhalimu Yazid, ndiyo iliyokuwa njia bora zaidi iliyodhamini maisha ya utukufu na heshima humu duniani na huko Akhera, na kudhalilishwa maadui humo duniani na Akhera.

Siku ya Ashura, Kashmir

 

Katika dua aliyosoma mwanzoni mwa mapambano yake, Imam Hussein (as) alisema: "Awe Mweyezi Mungu! Wewe unajua kwamba tuliyoyasema si kwa ajili ya kushindania madaraka na mali ya dunia bali lengo letu ni kurudisha Ishara za dini yako mahala pake na kurekebisha nchi yako ili waliodhulumiwa miongoni mwa waja wako wapate kuishi salama na kutekelezwa wajibu, sunna na sheria za dini yako."

Katika barua yake kwa watu wa Basra, Imam Hussein (as) pia alibainisha lengo la mapambano yake dhidi ya utawala dhalimu wa Yazid kwa kusema kwamba lengo lake kuu lilikuwa kuhuisha sunna za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Alisema: "Ninakuiteni katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake kwa sababu (kundi hili) limeharibu sunna hizo na kuhuisha bid'a." Anasema katika sehemu nyingine: "Wakati umma wa Kiislamu unapokabiliwa na utawala wa watu kama Yazid, Uislamu unapasa kusahaulika." Kwa maelezo hayo, mapambano ya Imam Hussein (as) yalikuwa ni mapambano ya marekebisho na ya kuamsha watu na kuwatoa kwenye giza la upotovu ambao ulikuwa umeenezwa miongoni mwa watu na utawala dhalimu wa Yazid. Hakika mtawala huyo fasidi alikuwa amepotosha kabisa dini ya Mtume (saw) na kuanzisha dini nyingine iliyokwenda kinyume na mafundisho sahihi ya Uislamu. Imam aliposema 'utawala wa watu kama Yazid' alikusudia kwamba si katika kipindi na zama hizo tu bali utawala fasidi na wa kidhalimu kama huo haupasi kuruhusiwa kabisa kutawala umma na jamii ya Kiislamu katika kipindi chochote kile cha historia. Imam (as) anasema katika sehemu nyingine: 'Mnapoona kuwa haki haitekelezwi wala batili kukatazwa, waumini wanapasa kusimama kwa ajili ya mapambano."

Tags