Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (10)
makala hii ya Maswali Kuhusu Tukio la Ashura leo itajibu swali kwamba, ni kwa nini hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake zimesisitiza sana suala la kuzuru kaburi la Imam Hussein bin Ali (as)?
Ni siri gani iliyomo katika kumzuru Imam Hussein bin Ali kiasi kwamba, mtu anayefanya amali hiyo Mwenyezi Mungu humpa malipo sawa na mtu anayehiji mara elfu na ujira wa mtu aliyeuliwa shahidi katika vita vya jihadi?
Katika utamaduni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia suala la kumzuru Imam Hussein bin Ali (as) linahesabiwa kuwa miongoni mwa ibada mustahabu zilizotiliwa mkazo kufanywa katika minasaba mbalimbali kama katika siku ya Ashuraa, siku ya Arubaini baada ya kuuliwa shahidi mtukufu huyo na masahaba zake, siku za idi na usiku wa kuamkia Ijumaa. Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume (saw) wamewahimiza waumini kumzuru Hussein (as) licha ya mashaka mengi waliyokuwa wakikumbana nayo kutoka kwa watawala madhalimu. Imepokewa kutoka kwa Imam Ja'far al Swadiq (as) kwamba amesema: Lau watu wangejua utukufu wa kuzuru kaburi la Imam Hussein (as) basi wangalikufa kwa shauku kubwa (ya kutaka kulizuru) na kuhatarisha maisha yao ili wapate fadhila hizo."
Vilevile imepokewa kutoka kwa Imam Muhammad al Baqir (as) kwamba amesema: Waamuruni wafuasi wetu kuzuru kaburi la Hussein bin Ali kwa sababu kumzuru huzidisha rizki, kurefusha umri na kuondoa balaa na mabaya..".
Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nini sababu na siri ya Maimamu katika kizazi cha Mtume (saw) kusisitiza sana suala la kuzuru kaburi la Imam Hussein (as)?
Maulamaa wakubwa wa madhehebu ya Suni kama Tirmidhii katika kitabu cha Sunan, al Haakim katika Mustadraku Sahihain, Haithami katika Majmaul Zawaidi, Ahmad bin Hanbal katika al Musnad, Bukhari katika kitabu chake cha al Adabul Mufrad, Ibn Majah katika Sunan na Tabarani katika al Muujamul Kabir wamenukuu hadithi ya Mtume Muhammad (saw) akisema: Hussein ni kutokana na mimi, na mimi natokana na Hussein, Mwenyezi Mungu ampende mwenye kumpenda Hussein..".
Yumkini hapa tukasema kuwa, adhama ya Ashuraa na siri ya fadhila na utukufu huo wote wa thawabu za kuzuru kaburi la Hussein bin Ali (as) zimo katika sentensi hiyo fupi lakini iliyojaa maana kubwa. Imam Hussein (as) alihuisha dini ya Mtume Muhammad (saw) baada ya kupotoshwa na kukaribia kuangamia na kwa msingi huo wanazuoni wa Kiislamu wanaamini kwamba, maana ya maneno ya Mtume (saw) yanayosema: Na mimi natokana na Hussein.." ni kwamba, harakati ya mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala na mapambano yake ya siku ya Ashuraa na hatimaye kuuawa kwake shahidi akiwa pamoja na masahaba zake vilihuisha tena jina la Uislamu na Mtume (saw) baada ya kupotoshwa na kukaribia kufutwa kabisa. Naam mapambano ya Hussein na kuuliwa kwake shahidi kuliunywesha mti wa Uislamu uliokuwa ukikauka kwa damu zao na kuhuisha tena risala ya Mtume na dini ya Mwenyezi Mungu. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana hadithi nyingi zikasisitiza sana suala la kuzuru kaburi la mtukufu huyo.
Kuzuru kaburi la Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (as) ni kutangaza tena utiifu wetu kwa Mtume (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake na kwamba tuko tayari kusabilia roho zetu, watoto wetu, mali zetu na kila tulichonacho kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu. Tunasoma katika ziara ya Imam Hussein kwamba: "Nitafanya suluhu na maafikiano na yule atakayefanya suluhu na nyinyi, na nitapigana vita na yeyote atakayewapiga vita nyinyi.." Vilevile tunasoma katika ziara ya Arubaini ya Imam Hussein kwamba: "Niko tayari kwa ajili ya kukunusuruni nyinyi.." Kwa hakika maneno haya yana maana ya kutoa tena mkono wa utiifu kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu na kutangaza waziwazi kwamba, tuko tayari kusabilia kila tulichonacho kwa ajili ya kunusuru Uislamu na matukufu yake. Naam, hii ndiyo siri ya thawabu za kumzuru Hussein (as) ambaye ndiye kinara wa harakati hiyo ya kuhuisha tena Uislamu na kulinda matukufu yake kwa hali na mali. Hii ndiyo maana ya kauli ya Mtume (saw) iliyopokewa na wanazuoni wa Kiislamu kwamba: Hussein ni kutokana na mimi, na mimi natokana na Hussein.
Kubeba mashaka ya safari ya kwenda kuzuru kaburi la Imamu na kinara wa wapigania haki, uadilifu na dini ya Allah, Hussein (as), kuwa tayari kukabiliana na matatizo yote ya safari hiyo na kufanya ibada, dua na kumtaradhia Mwenyezi Mungu mmoja kandokando ya makaburi ya mashujaa waliopigania dini yake na kusabilia roho zao kwa ajili yake huzusha hamasa kubwa na ya aina yake katika nafsi ya mtu anayekwenda kufanya ziara. Hamasa hiyo ndiyo ile ile iliyoshuhudiwa katika nyoyo za ansari na masahaba wa Imam Hussein (as) siku ya tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria ambayo haina kifani katika historia ya mwanadamu.
Kuzuru kaburi la Hussein (as) pia ni kielelezo cha kutafuta wasila na njia inayomkurubisha zaidi mja kwa Mola wake Karima. Aya ya 35 ya Suratul Maida inasema: Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikilia. Na wanieni kwa juhudi kwa ajili yake ili mpate kuokoka.
Wasila na njia inayotajwa katika aya hii ina maana pana zaidi, na kila kitu au amali inayomkurubisha zaidi mja kwa Mola wake inatambuliwa kuwa ni wasila na njia ya kumfikisha kwa Allah SW. Njia na wasila muhimu zaidi ni imani ya Tauhidi na Mungu Mmoja na kumsadikisha Mtume wake Muhammad (saw) na kuwa na imani ya Siku ya Malipo na Kiyama huko Akhera. Njia hizo zinapaswa kufuatiwa na kumcha Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza maamrisho yake na kujipesha na makatazo yake, kupigana jihadi katika njia yake na kadhalika. Shufaa na maombezi ya Mitume, maimamu na waja wema wa Mwenyezi Mungu pia ni miongoni mwa mambo yanayomkurubisha mja kwa Mola Karima kama inavyoashiria aya ya 97 ya Suratu Yusuf pale ndugu wa mtukufu huyo walipomwendea baba yao, Nabii Yaaqub na kumuomba awaombee maghufira na msamaha kwa Mola Muweza kutokana na madhambi waliyokuwa wamemfanyia ndugu yao, na Nabii Yaquub akakubali kufanya hivyo.
Ni vyema hapa kuashiria kuwa, kwa mujibu wa hadithi sahihi zilizopokewa na maulama wa Kiislamu, maasumina na mawalii wa Mwenyezi Mungu wanashuhudia amali na matendo yetu na hakuna tofauti kwao baina ya kuwa wako hai hapa duniani au wameaga dunia. Tabarani amepokea katika kitabu cha al Muujamul Kabir kwamba Mtume (saw) amesema: Mtu anayefanya Hija kisha akazuru kaburi langu baada ya kuwa nimeaga dunia huwa sawa na yule aliyenizuru mimi nikiwa hai, na mimi nitakuwa muombezi na shafii wake Siku ya Kiyama.
Hapa inabainika kuwa, kumzuru Mtume (saw) na Maimamu katika kizazi chake kitukufu ni wasila na njia ya kutukurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kututia hamasa ya kuwa tayari kusimama kidete na kusabilia roho zetu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na dini yake.