Zama za Mitandao ya Kijamii, Faida na Madhara Yake
(last modified Sun, 02 Jul 2023 13:18:27 GMT )
Jul 02, 2023 13:18 UTC
  • Zama za Mitandao ya Kijamii, Faida na Madhara Yake

Kupanuka na kuenea kwa mitandao ya kijamii kuna nafasi muhimu katika maisha ya kila siku ya wanadamu, hasa tabaka la vijana. Tarehe 30 mwezi wa Juni ni Siku ya Mitandao ya Kijamii Duniani; kwa msingi huo tunatumia fursa hii kuchunguza umuhimu na athari chanya na hasi za mitandao hiyo kwa jamii na maisha yetu.

Kupakua na kuweka programu za mitandao ya kijamii kwenye simu, runinga na kadhalika kunahesabiwa kuwa hatua ya kwanza na rahisi zaidi ya kuingia kwenye ulimwengu pepe (virtual world) ambao siku hizi watu wengi wamezama ndani yake. Ulimwengu pepe, kama zilivyo teknolojia nyingine nyingi zinazotengenezwa na binadamu, una faida na hasara zake maksusi. 

Miongoni mwa athari chanya za mitandao hiyo kwa maisha ya kila siku ya watu ni kupata taarifa na habari za hivi punde, kujaza wakati wa bure, kuwasiliana kirahisi na familia na marafiki, na kuunda vikundi vya kirafiki, kikazi na kadhalika. Katika mitandao hiyo ya kijamii watu wanaweza kuwasiliana kwa urahisi na wapendwa wao walioko katika kona zote za duniani na kupata habari zao.

Mitandao ya kijamii  

Hata hivyo hii sio hadithi na kisa kizima cha mitandao ya kijamii. Leo, hebu tuachane na nukta hizi nzuri za mitandao ya kijamii na tujikite zaidi kwenye matumizi yasiyo sahihi ya mitandao hiyo. Labda kwa mtazamo huu, tunaweza kutumia vyema mitandao hiyo na nyenzo zake, na kuweka ratiba nzuri zaidi ya utumiaji wa mitandao ya kijamii. Ni dhahiri kwamba iwapo mitandao ya kijamii itatumiwa vizuri na kwa tahadhari katika njia ya ustawi na maendeleo yetu na jamii kwa ujumla, tutapata faida nyingi na kupunguza athari zake mbaya.

Hii leo, mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya muundo wa mawasiliano, na wakati huo huo miongoni mwa sababu muhimu zaidi za mabadiliko yanayoshuhudiwa katika mtindo wa maisha, ambayo yameathiri jinsi watu wanavyozungumza, jinsi wanavyojikwatua na kuvaa, nyakati zao za kulala na kupumzika na kadhalika. Mbali na mtindo wa maisha, mitandao ya kijamii imeweza kuibua maadili mapya au mifumo ya thamani ambayo imeonekana katika mifumo ya kitamaduni ya tabia za watu.

Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vina sifa nyingine muhimu, ikiwa ni pamoja na kwamba vimewafanya watazamaji na wafuatiliaji wengi wa vyombo vya habari kuwa wanaharakati katika tasnia hii ya habari na mawasiliano, utayarishaji na usambazaji wa habari sasa haudhibitiwi tena na vyombo maalumu vya habari, na kila mtumiaji anaweza kuzalisha na kuzambaza habari zake. Hapana shaka kuwa, sambamba na faida hizi, uwezekano wa kueneza habari zisizo za kweli au zenye madhara pia umeongezeka, na walengwa wa vyombo vya habari vya jadi wamepungua, huku wafuatiliaji wa habari zisizo makini wakiongezeka.

Miongoni mwa matokeo muhimu zaidi ya janga la mitandao ya kijamii ni kuhatarisha afya ya akili na kinafsi ya watumiaji wake. Utafiti uliofanywa na watafiti wa tabia na sayansi ya jamii unaonyesha kuwa, kuna uhusiano mkubwa kati ya matumizi yasiyofaa na ya kupita kiasi ya mitandao ya kijamii na matatizo ya kiakili na kisaikolojia; na mitandao ya kijamii inaweza kusababisha matatizo katika afya ya akili ya watu ambayo wakati mwingine hayawezi kufidiwa.

Katika ulimwengu wa sasa, wengi wetu tunategemea mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Snapchat, YouTube, Tik Tok, na Instagram kutafuta jambo au kuwasiliana. Pamoja na hayo ni muhimu kutambua kuwa mitandao ya kijamii haiwezi kamwe kuchukua nafasi ya mawasiliano halisi na ya moja kwa moja baina ya binadamu. Imethibiti kuwa, ili kuamsha homoni zinazoondoa mkazo na msongo wa mawazo na kutufanya tuwe na furaha, afya na utanashati zaidi, tunahitaji kuwasiliana ana kwa ana na wanadamu wengine. Jambo jingine ni kwamba, katika teknolojia hii iliyoundwa ili kuwakurubisha watu zaidi, kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kunaweza kutufanya tujihisi wapweke zaidi na tujitenge, na kuzidisha matatizo ya afya ya akili kama vile mfadhaiko na sonona.

Hebu tutoe mifano ya hisia zinazosababishwa na utumiaji uliopindukia wa mitandao ya kijamii ndani ya nafsi zetu: Miongoni mwa hisia hizo ni ile ya kutoridhika na maisha na mwonekano wako. Hata pale tunapojua kwamba picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimechujwa au kubadilishwa kwa kutumia programu makhsusi kama photoshop, bado picha hizo zinaweza kutufanya tuhisi kutojiamini na kuvunjwa moyo na mwonekano au aina na hali ya maisha yetu. Tunajua kwamba watu huwashirikisha wenzao mambo na matukio chanya na mazuri ya maisha yao katika mitandao ya kijamii, na ni mara chache sana kuona watu wakionyesha masuala hasi na hisia zao zisizofurahisha katika mitandao hiyo. Pamoja na hayo, tunapotazama mambo ya kupendeza ya maisha ya watu wengine, yumkini kukazusha hisia za husuda, hasira, kulinganisha au majuto ndani nafsi za baadhi ya watu na kuhatarisha afya yao ya akili na nafsi.

Mfano mwingine wa hisia zinazosababishwa na utumiaji uliopindukia wa mitandao ya kijamii ni kujenga hali ya kupenda kujitenga na watu. Wengi wetu tunaweza kuhisi kuwa tumeunganishwa na watu wengi kutokana na kutumia mitandao ya kijamii, na kwamba kila tunapowasha na kuingia kwenye mitandao hiyo, huwa hatuko peke yetu. Hata hivyo utafiti umeonyesha kuwa, kutegemea sana mahusiano katika mitandano ya kijamii, badala ya mawasiliano halisi ya moja kwa moja, kunazidisha hisia ya kujitenga na kumfanya mtumiaji awe mbali na mawasiliano halisi. Matokeo yake, matatizo ya kimienendo, wahka na sonona yanaweza kujitokeza kutokana na kutokuwa katika jamii halisi na kutokuwepo kwa mawasiliano yenye ufanisi, mfungamano wa karibu na kadhalika; suala ambalo yumkini likawa na taathira mbaya kwa afya ya akili.

Kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii na kuwa mraibu wa mazingira hayo, bila shaka, kuna athari mbaya na kubwa kwa afya ya akili, na huenda muhimu zaidi kati ya madhara na taathira hizo ni tatizo la sonona na msongo wa mawazo. Watu ambao wana dalili za sonona (depression) kutokana na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii, mara nyingi huripoti ukosefu wa usingizi mzuri, lishe bora, na mawasiliano halisi na yenye ufanisi; na mambo haya hatimaye huwaweka mbali na malengo na maslahi yao, na badala yake kuwatumbukiza katika hali ya kupenda kujitenga, kupoteza matumaini na msongo wa mawazo.

Utegemezi wa ulimwengu pepe na mitandao ya kijamii huwafanya watu wajikite na kuelekeza mazingatio yao kwenye kazi na maoni ya watu wengine, na badala ya kuzingatia mipango na malengo yao wenyewe, ambayo yanalingana na suhula na hali zao, wanaunganisha fikra na akili zao na mitandao hiyo na mwishowe, hutumbukia katika matatizo ya sonona kali na matatizo mengine mengi ya kinafsi na kiakili.   

Sonona ni miongoni mwa matokeo mabaya ya uraibu wa mitandao ya kijamii.

Mwishoni mwa kipindi chetu cha leo, tutupie jicho baadhi ya mbinu za kupunguza uharibifu unaosababishwa na mitandao ya kijamii kwenye afya ya akili.

Jaribu kupunguza wakati na mahali pa kutumia mitandao ya kijamii. Utakuwa na mawasiliano bora na watu maishani mwako iwapo arifa zako za mitandao ya kijamii zitazimwa nyakati fulani za mchana, au ikiwa simu yako itakuwa kwenye hali ya ndegeni (airplane mode) nyakati fulani, kama vile usiku. Jitolee kutoangalia mitandao ya kijamii unapokula chakula na familia na marafiki, kucheza au kuzungumza na watoto. Usiweke simu au kompyuta yako kwenye chumba cha kulala kwani jambo hili litavuruga na kuharibu usingizi wako.

Weka utaratibu wa mara kwa mara kuachana na mitandao ya kijamii kwa siku kadhaa. Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa hata mapumziko ya siku tano au wiki moja kutoka kwenye Facebook, Instagram nk .. yanaweza kupunguza msongo wa mawazo na kukufanya uridhike zaidi na maisha. Utafiti umeonyesha kuwa kupunguza matumizi ya kila siku ya Facebook, Instagram na Snapchat hupelekea kupungua upweke, mfadhaiko na sonona. Mwanzoni jambo hili linaweza kuwa gumu, lakini hatua kwa hatua, mazoezi ya tabia hii yanaweza kuchukua nafasi ya matumizi ya kila siku ya mitandao ya kijamii.

Tovuti ya habari za afya "Net Medicine" inasema kuwa, katika utafiti mmoja, wanafunzi walipunguza na kubana matumizi yao ya mitandao ya kijamii kwa wiki mbili. Ella Falber, mtafiti mkuu kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa anasema: Watafiti walipowauliza washiriki kuhusu uzoefu wao, walipata majibu ya kuvutia. Wengi wao walisema walitatizika hapo mwanzoni, lakini baadaye waliona jinsi walivyolala vizuri na jinsi walivyokuwa wamefanya mawasiliano zaidi na watu katika maisha halisi.

Unapotumia mitandao ya kijamii au kabla na baada, jaribu kuzingatia hisia unazopata na kujua aina yake. Wengi kati ya watu na watumiaji wa mitandao ya kijamii wameripoti kuwa, kutokana na utumiaji mwingi na mkubwa wa mitandao ya kijamii, hawapati hisia za kufurahisha na hupuuza mipango yao ya kila siku na hali zao wao wenyewe. Hivyo basi, ni bora kuweka wazi na kujua sababu ya kutumia mitandao ya kijamii, ili uweze kutumia anga hiyo kwa madhumuni maalumu na usiwe mbali na mipango yako binafsi katika ulimwengu halisi.

Kutumia mitandao ya kijamii kwa ajiilii ya kujuliana hali na ndugu, jamaa na marafiki kama burudani au kutoa maoni yanayofaa na kadhalika ni jambo zuri, kwa sharti kwamba kusikuzuiye kuwatembelea na kukutana nao ana kwa ana baada ya muda. Kutuma ujumbe kwenye Twitter kwa mfanyakazi mwenzako kunaweza kuwa jambo zuri na la kufurahisha, lakini hakikisha kwamba mawasiliano haya hayachukui nafasi ya mazungumzo ya ana kwa ana.

Kumbuka kwamba tunapotumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kwa uelewa, majukwaa haya yanaweza kuwa nyongeza muhimu kwa maisha yetu ya kijamii. Hata hivyo ni mwanaadamu halisi tu na mawasiliano ya moja kwa moja na mwanaadamu mwenzako aliyeketi mbele yako ndiyo yaanaweza kukidhi mahitaji yako ya msingi.