Serikali ya Tanzania yaweka pingamizi kesi ya kupinga uwekezaji bandarini
Serikali ya Tanzania imeweka mapingamizi katika kesi iliyofunguliwa na mawakili wanne kupinga uwekezaji wa bandari za nchi hiyo na kuitaka Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya iitupilie mbali kwa madai kwamba iko kinyume cha sheria na Katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mapingamizi hayo yamewasilishwa mahakamani kwa njia ya maandishi na Wakili Mkuu wa Serikali Dk. Boniphace Luhende akijibu hoja za mawakili hao wanne waliofungua kesi hiyo akiwemo Alphonace Lusako na Emmanuel Chengula ambao wanawakilishwa na Wakili Boniface Mwabukusi na wenzake.
Mawakili hao wamefungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Bunge.

Kesi hiyo ilifunguliwa muda mfupi baada ya mkataba wa ushirikiano wa kiserikali kati ya Tanzania na Dubai, kuhusu uendeshaji, usimamizi na uendelezaji bandari kuridhiwa na Bunge la nchi hiyo.
Mapingamizi hayo yanatarajiwa kusikilizwa wakati kesi itakapoanza kusikilizwa mfululizo, kuanzia tarehe 20 Julai, mbele ya Jopo la Majaji Watatu, Jaji Abdo Kagomba, Jaji Ndunguru na Jaji Mustafa Kambona.
Waliofungua kesi hiyo wanadai baadhi ya vipengele vya mkataba huo vinakiuka Katiba ya nchi, kupelekwa bungeni kuridhiwa bila kushirikisha umma na kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutoa maoni yao.../