Waislamu wa Kishia Nairobi Kenya waandamana katika kumbukumbu ya Ashura
Waislamu wa madhehebu ya Shia mjini Nairobi, mji mkuu wa Kenya walikusanyika kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as) katika siku ya Ashura.
Waislamu hao wa Kishia wakiandamana katika kumbukumbu ya Ashura walisika wakipiga nara za Labbayka ya Hussein na kuonyesha mapenzi yao makubwa kwa Imamu Hussein na Ahlul Bayt (as). Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji mingine ya Kenya kama Lamu.
Maandamano hayo ya kumbukumbu ya Ashura nchini Kenya kwa mara nyingine tena yanathibitisha kuwa na nafasi muhimu miongoni mwa Wakenya mafundisho ya Ahlul-Bayt, sira na harakati ya Imamu Hussein (as) iliyokuwa na lengo la kupinga dhulma na kutetea Uislamu.
Wakati huo huo katika nchi ya jirani ya Tanzania pia, mikoa mbalimbali ikiwemo ya Arusha, Singida, Tanga, Dar es Salaam, Kigoma, Pwani na kwingineko, imeshuhuudia kufanyika pia mandamano ya kumbukumbu ya Ashura ambapo waandamanaji wameonyesha huba na mapenzi yao makubwa kwa Imamu Hussein (as) na Ahlul-Bayt (as).

Aidha katika baadhi ya maandamano hayo, waandamanaji sambamba na kuomboleza kumbukumbu ya kifo cha Imamu Hussein wamelaani pia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko nchini Sweden na Denmark.
Wakati huo huo, Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma nchini Tanzania kwa pamoja wamelaani vikali kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani.
Katika mkusanyiko wao wa pamoja, Waislamu hao wakiwa na mabango yaliyoandikwa: Ewe Dunia, Qur'ani yetu ni mstari mwekundu" wamesisitiza kwamba, katu hawakubaliani na kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani tukufu kitabu ambacho wameeleza kuwa ni katiba ya Waislamu.