Wakimbizi 16 wakufa maji baada ya boti zao kuzama Kaskazini mwa Afrika
(last modified Tue, 08 Aug 2023 07:32:13 GMT )
Aug 08, 2023 07:32 UTC
  • Wakimbizi 16 wakufa maji baada ya boti zao kuzama Kaskazini mwa Afrika

Wahajiri wasiopungua 11 wamepoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika maji wa Bahari ya Mediterrania, pwani ya Tunisia.

Hayo yamesemwa na Faouzi Masmoudi, Msemaji wa Mahakama ya mji wa bandari wa Sfax ambaye ameongeza kuwa, miili mingine saba imeopolewa majini na kuongeza idadi ya wakimbizi walioaga dunia kwenye ajali hiyo kufikia 11. 

Amesema boti hiyo iliyozama mwishoni mwa wiki karibu na visiwa vya Kerkennah kwenye Bahari ya Mediterrania ilikuwa imebeba wahajiri 57; wote wakiwa ni raia wa nchi za eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.

Afisa huyo wa Idara ya Mahakama ya Tunisia amebainisha kuwa, wahajiri wawili tu ndio wameokolewa kufikia sasa na wapigambizi wa Gadi ya Pwani ya Tunisia kwenye tukio hilo.

Katika hatua nyingine, mamlaka za Morocco hapo jana zilitangaza habari ya kuopolewa maiti tano za wakimbizi kutoka Senegal, katika pwani ya Sahara Magharibi.

Wahajiri wa Kiafrika pwani ya Tunisia

Inaarifiwa kuwa, wahajiri 189 wameokolewa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuelekea Italia kuzama katika maji wa Bahari ya Mediterrania, pwani ya eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi.

Kwa mujibu wa televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, hali ya mamia ya wahajiri wa Kiafrika waliokwama katika eneo la mpaka wa Tunisia na Libya inazidi kuwa mbaya baada ya kufukuzwa na mamlaka ya Tunisia kutoka kwenye mji wa Sfax, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Tunisia iko kwenye eneo la katikati mwa Bahari ya Mediterania, na ni moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahamiaji haramu wenye tamaa ya kufika barani Ulaya.