Waasi wa ADF wameua watu 55 DRC ndani ya wiki 2
(last modified Tue, 15 Aug 2023 07:40:31 GMT )
Aug 15, 2023 07:40 UTC
  • Waasi wa ADF wameua watu 55 DRC ndani ya wiki 2

Waasi wa kundi linalojiita Allied Democratic Forces (ADF) wamewaua makumi ya wanavijiji huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Kinos Katuo, rais wa jumuiya moja ya kiraia katika kitongoji cha Mamove mjini Beni amesema waasi hao wamelenga vijiji kadhaa kwenye mashambulio hayo katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini.

Amesema, "Kuanzia Julai 31 hadi Agosti 14, watu 55 wameuawa na waasi wa ADF na waitifaki wao. Katika eneo la Batangi-Mbau mjini Beni, watu 19 waliuawa ndani ya usiku mmoja."

Katuo amesema vijiji vilivyoshambuliwa na waasi wa ADF ndani ya wiki mbili zilizopita ni Mbingi, Makangwa, Mabuo, Moliso, Masia na Masenze, huku akiwakosoa vikali wanavijiji wanaoshirikiana na waasi hao kutenda jinai hizo.

Naye Luteni Pecos Mboka, afisa usalama katika mkoa wa Ituri amethibitisha habari ya kutokea mauaji hayo akieleza kuwa, waasi hao wamekuwa wakilenga vijiji ambavyo havina wanajeshi.

Waasi wa ADF

Hata hivyo anasisitiza kuwa, kwa ujumla mashambulizi katika maeneo hayo yamepungua kwa kiasi kukubwa, hasa katika maeneo ambayo vikosi vya pamoja vya DRC na Uganda vimekita kambi.

ADF ni moja ya makumi ya makundi yenye silaha yanayoeneza vurugu mashariki mwa Kongo, mengi yakiwa ni urithi wa vita vya kikanda vilivyopiganwa baada ya kuanguka kwa dikteta wa muda mrefu wa taifa hilo la Afrika, Mobutu Sese Seko katika miaka ya 1990.

 

Tags