Sep 15, 2024 11:57 UTC
  • Wanaharakati DRC wakaribisha kuhukumiwa kifo raia wa US

Wanaharakati, wanasiasa na watetezi wa haki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameipongeza Mahakama ya Kijeshi ya nchi hiyo kwa kuwahukumu kifo watu 37 wakiwemo raia watatu wa Marekani na mmoja wa Uingereza, baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na jaribio la kuipindua serikali katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika, Juni mwaka huu.

Katika mahojiano ya kipekee na shirika la habari la Iran Press, Espoir Muhinuka, kiongozi wa mashirika ya kiraia mjini Goma, amekaribisha uamuzi huo, na kuutaja kama kama ujumbe wenye nguvu kwa Marekani na maajinabi wengine.

Amesema kuwa hukumu hiyo ni nukta muhimu katika historia ya DRC, akisisitiza azma ya nchi hiyo ya kulinda taasisi zake dhidi ya kuhujumiwa na nchi za nje.

Muhinuka ameeleza kuwa, uamuzi huu unaonyesha kuwa DRC haiogopi tena ushawishi wa Marekani, na ni onyo kwa mataifa ya Magharibi yanayotaka kulihujumu taifa hilo.

Kwa upande wake, Leopold Baguma, mwanachama mwandamizi wa chama cha Alliance of Democratic Forces of Congo (AFDC), pia amepongeza uamuzi wa mahakama katika mahojiano maalum na Iran Press. Amesisitiza ulazima wa Marekani kuheshimu uhuru wa nchi za Afrika, akisisitiza kwamba hukumu hiyo inaonyesha azma na irada ya Kongo wa kuwawajibisha raia wa kigeni licha ya mashinikizo ya kimataifa.

Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Naye Georges Yalala, mwanachama wa Muungano wa Demokrasia na Ustawi wa Kijamii (UDPS), chama cha Rais Felix Tshisekedi ameunga mkono ushujaa wa mfumo wa haki wa Kongo. Ameionya Marekani dhidi ya jaribio lolote la kuiyumbisha DRC katika siku za usoni , akisisitiza kuwa nchi hiyo sasa ina uwezo wa kulinda demokrasia na uhuru wake kutoka kwa ushawishi wa kigeni.

Kadhalika aghalabu ya wananchi wa DRC hususan wakazi wa jiji la Goma la mashariki mwa nchi wamepongeza na kufurahia hukumu hiyo.

Tags